Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Namba ya dharura

Polisi nchini Marekani wamemkamata na kumshitaki bwana mmoja kwa kutumia vibaya namba ya simu ya dharura.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Simu

Mtandao wa cnews.com umesema polisi walimshitaki Bwana Raymond Roberge mwenye umri wa miaka 65, kwa kupiga simu hiyo, namba 911.

Bwana huyo alipiga simu hiyo na kusema amepatwa na dharura, na alipoulizwa dharura gani, alijibu kuwa ameishiwa bia alizokuwa anakunywa. Taarifa zinasema bwana huyo wa mjini Bridgeport, Connecticut, alipiga simu mara tatu, akiomba kutatuliwa dharura yake hiyo.

Gazeti la Connecticut Post pia limeripoti kuwa hii si mara ya kwanza kwa Bwana Raymond kufanya hivyo, kwani amekwishawahi kupiga simu huyo pasipo na dharura rasmi, takriban mara themanini.

Aua chura wa jirani

Bwana mmoja nchini Ujerumani amefikishwa mahakamani siku ya Alhamisi, baada ya kuwapiga risasi na kuwaua vyura wawili wa jirani yake.

Image caption Chura

Gazeti la Rheinische Post limesema bwana huyo aliwapiga risasi vyura wa jirani yake saa nane usiku.

Mmoja wa vyura hao alifariki papo hapo, na chura mwingine kufariki kesho yake. Taarifa zinasema, majirani hao, wote wana mabwawa ya maji, ingawa mmoja ana vyura wake na mwingine hana. Aidha habari zaidi zinasema, mara nyingi katika msimu wa kuzaliana, vyura hupiga kelele usiku, kama ilivyokuwa katika tukio hilo.

"Nilisikia mlio wa bunduki, na mara moja nikajua kilichotokea," amesema Andreas van Straelen, ambaye vyura wake walipigwa risasi. Alikwenda nje na kukuta vyura wake wakiwa na matundu ya risasi. Alimchukua mmoja wa vyura hao na kumuweka katika friji, kama ushahidi. Mtuhumiwa amegoma kusema lolote kuhusiaa na sakata hilo.

Wezi waiba nyuki

Maelfu kadhaa wa nyuki, waliokuwa wakifungwa katika mradi wa mamilioni ya dola wa kitafidi wameibiwa katika chuo kikuu kimoja hapa Uingereza.

Image caption Nyuki

Polisi katika eneo la Tayside la Scotland wametoa wito siku ya Jumanne kuomba wananchi kutoa tarifa kuhusu mizinga minne ya nyuki yenye maelfu ya nyuki weusi walioibwa kutoka chuo cha kitabibu mjini Dunde. "Wizi huu utatatiza sana utafiti wetu," amesema Dokta Chris Connolly, mkuu wa utafiti huo. Taarifa iliyotolewa imesema nyuki hao ni wa kipekee, na ni rahisi kutambulika iwapo wataonekana wakiuzwa.

Dokta Connolly amesema huenda nyuki hao wameibiwa ili wapelekwe kuzaliana zaidi, au kwenda kuuzwa kwa wataalam wa ufugaji nyuki. "Yeyote aliyefanya hivi, lazima anafahamu mengi kuhusu nyuki" amesema Dokta Connolly.

Unyumba wamfikisha kizimbani

Haki miliki ya picha BBC One
Image caption Mwanamke kakasirika (sio huyu lakini)

Mwanamama mmoja huko Dubai anamshitaki mume wake wa zamani, kwa kushindwa kumtaarifu mapema kuwa hawezi kutoa unyumba, kabla hawajafunga ndoa.

Gazeti la Hundustan Times limesema mwanamama huyo amewasilisha kesi ya madai ya dola milioni kumi na moja.

Amesema amepata athari ya kiakili kutokana na tukio hilo. Mwanamama huyo amedai kuwa, alipoolewa, mume wake alimlazimisha kucha kazi aliyokuwa akifanya, na kuuza vito vyake vyote vya thamani. Licha ya hivyo Mwanaume huyo hakumpa haki yake ya ndoa.

Taarifa zinasema baada ya miezi minne, mwanamama huyo aligundua kuwa mume wake huyo jongoo halipandi mtungi na kulazimika kudai talaka. "Kwa kuzingatia misingi ya Kiarabu, na nafasi ya mwanamke katika jamii, nilibaki kimya na kujaribu kumuomba Mungu labda mambo yatakaa sawa" amesema mwanamama huyo akizungumza na gazeti la Hundustan.

Muda zaidi wa jela

Kijana mmoja mhalifu nchini Canada amemuomba hakimu ampe adhabu zaidi ya kukaa gerezani, ili aweze kuwa karibu na mfungwa mwenzake, ambaye ni baba yake wa kambo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Jela

Justin Beynen mwenye umri wa miaka 18 alipewa hukumu ya miezi sita jela kutokana na makosa mbalimbali, lakini alimuomba jaji ampe muda zaidi, ili akae na baba yake Jason Hastings ambaye na yeye yuko jela.

Kijana Beynen alimuambia hakimu Normand Glaude kuwa hatakuwa na mahala pa kwenda akitoka jela mapema, hadi baba yake huyo atakapoachiliwa kutoka jela mwezi Oktoba. Hakimu Glaude alisema mahakama sio shirika la jamii, lakini hata hivyo alipa kijana huyo muda anaotaka wa kukaa gerezani.

Nyama ya mtu

Polisi nchini Slovakia walifanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyekuwa akielekea kula nyama y binaadam siku ya Jumanne. Waziri wa mambo ya ndani wa Slovakia, Daniel Lipsic amesema katika mji wa Kysak, kaskazini mashariki mwa Slovakia.

Mapambano ya bunduki kati ya bwana huyo na polisi yalizuka, wakati mshukiwa akikabiliana na polisi, huku polisi mmoja alijeruhiwa. Polisi waliweza kutambua njama hizo, baada ya kugundua barua pepe kati ya mla nyama ya binaadam, na mtu mmoja raia wa Uswisi, aliyekuwa akitaka mwili wake uliwe.

"Bwana huyo wa Usiwsi alikuwa akitaka kufa, na wakakubaliana kuwa mwili wake ukatwekatwe na uliwe" amesema waziri Lipsic, akikaririwa na shirika la habari la Uchina, Xinhua.

Na kwa taarifa yako

...Moyo wako unadunda zaidi ya mara laki moja kwa siku...

Tukutane wiki ijayo.... Panapo majaaliwa...