Misri inachelewesha mkataba wa Mto Nile

Baada ya mazungumzo ya masaa baina ya serikali mpya ya Misri na Ethiopia, kuhusu swala tete la kugawana maji ya Mto Nile, makubaliano yamefikiwa kuwa Ethiopia haitotia saini ya mwisho ya mkataba mpya wa Mto Nile, hadi serikali mpya ya Misri itaposhika madaraka na kujiunga na mazungumzo hayo.

Mto Nile ndio maisha ya Misri, ndio chanzo pekee cha maji cha nchi hiyo.

Jambo hilo lilitambuliwa kwenye mkataba wa mwaka 1929 baina ya Uingereza na Misri, ambao ulisema hakuna mabadiliko yoyote yatakayofanywa kwenye Mto Nile, ambayo yatapunguza maji yanayofika Misri.

Mkataba huo uliithibitishia Misri kuwa itapata thuluthi mbili ya maji ya Mto Nile daima.

Katika miaka ya karibuni, nchi nyengine kando ya Nile zilikataa mkataba huo wa kikoloni.

Mwaka jana, baada ya juhudi za mwongo mzima kujaribu kubadilisha msimamo wa Misri kushindwa, nchi 6 za Nile zilikubaliana kutayarisha mkataba mwipya ambao Rais Mubarak aliupinga kabisa.

Ndio sababu ya Waziri Mkuu mpya wa Misri Essam Sharaf, kuzuru Ethiopia.

Baada ya mazungumzo, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi alitangaza kuwa nchi yake haitotia saini mkataba mpya hadi serikali mpya ya Misri itapochukua madaraka kufuatia uchaguzi.

Hiyo itamaanisha kuwa Ethiopia itabidi kusimamisha ujenzi wa bwawa muhimu.