Mzozo wa katiba unasuluhishwa Zimbabwe

Vyama vya Zimbabwe vimetatua mzozo kuhusu matayarisho ya katiba mpya ya nchi.

Haki miliki ya picha AFP

Mazungumzo hayo yalivunjika mapema juma hili kuhusu namna ya kushirikisha maoni ya watu wa kawaida kwa kuwashauri nchini kote Zimbabwe.

Msemaji wa chama cha Waziri Mkuu, Morgan Tsvangirai, aliiambia BBC, tatizo hilo sasa limeondoka.

Katiba mpya inatarajiwa kutayarishwa ufikapo mwezi Septemba, na msemaji huyo, Douglas Mwonzora, alieleza bado ana matumaini kuwa lengo hilo litafikiwa iwapo polisi wataacha kubughudhi chama chao.

Kufwatana na mkataba wa amani kati ya wanasiasa wa Zimbabwe, ulioongozwa na Afrika Kusini, katiba mpya inahitajika kabla ya uchaguzi kufanywa.