Mkwamo katika vita vya Libya

Mkuu wa jeshi la Uingereza, Jenerali Sir David Richards, ameihimiza NATO kuzidisha shughuli zake za kijeshi nchini Libya kwa kushambulia maeneo zaidi, ambayo inaruhusiwa kuyalenga.

Haki miliki ya picha AFP

Akihojiwa na gazeti moja la Uingereza, The Sunday Telegraph, alisema kama NATO haikufanya hivo basi itashindwa, na Kanali Gaddafi atabaki madarakani.

John Nichol aliwahi kuwa rubani wa jeshi la wanahewa la Uingereza, RAF, ambaye alidunguliwa Iraq katika vita vya kwanza vya Ghuba.

Anasema matamshi ya Jenerali Richards yanaonesha kuwa kunahitajika mkakati mwengine, ama sivyo, kuna hatari kuwa NATO itakwama kwenye operesheni ya Libya, ambazo zitakwama kwa miaka:

"Sote tunaotazama hali hivi sasa tunajua, kweli tumewawahifadhi raia, na hilo ni jambo jema.

Hayo tunakubaliana.

Lakini jee, sasa tutafanya nini?

Tumewalinda raia kwa siku 57; hata hivo mamia au pengine maelfu wamekufa.

Lakini sasa tufanye nini?

Hichi kipengee cha kulinda mstari wa mbele hakifai, kwa sababu kuna watu wanaendesha malori kwenye bara-bara kuu na kuuwana.

Kuna wenye ufundi wa shabaha wanaotumia bunduki.

Bado kuna vikundi vinavouwa watu.

Tufanye nini?

Au tubaki kwenye mkwamo, huku majeshi ya wanahewa ya Uingereza, Utaliana na Ufaransa yakilinda upande mmoja wa nchi, huku serikali inadhibiti upande mwengine.

Na mkwamo huo unaweza kuendelea kwa miaka."