ICC yataka hati ya kukamatwa kwa Gaddafi

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Libya

Mwendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC inataka kutoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi na wengine wawili kwa uhalifu dhidi ya binadamu.

Luis Moreno-Ocampo alisema Kanali Gaddafi, mtoto wake wa kiume Seif al-Islam, na mkuu wa idara ya ujasusi Abdullah al-Sanusi wamehusika kwa "mashambulio yaliyopangwa kwa ufanisi na kutapakaa" kwa raia.

Majaji wa ICC bado wanatakiwa kuamua iwapo watoe hati ya kukamatwa kwao au la.

Serikali ya Libya tayari imesema itapuuza hatua hiyo.

Naibu waziri wa mambo ya nje Khalid Kaim alisema mahakama hiyo ni "mtoto wa Umoja wa Ulaya ulioandaliwa kwa ajili ya wanasiasa na viongozi wa Afrika" na shughuli zake "zinatia shaka".

Alisema, Libya haikuitambua mahakama hiyo, kama ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika na Marekani, na itapuuza tangazo lolote.