Afya ya mke wa Bw Mubarak yaridhisha

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Bi Suzanne Mubarak

Mke wa Rais wa Misri aliyeondolewa madarakani Hosni Mubarak anaendelea kupata nafuu hospitalini kufuatia kuugua baada ya kuambiwa atatiwa kizuizini wakati wa kuhojiwa juu ya ulaji rushwa.

Ripoti za awali zilisema Suzanne Mubarak, mwenye umri wa miaka 70, alipata mshtuko wa moyo lakini baadhi ya maafisa wamesema alishikwa na "woga".

Hali ya Bi Mubarak imeimarika katika hospitali ya Sharm el-Sheikh.

Bw Mubarak anakabiliwa na madai ya "kupata mali kinyume cha sheria". Bw Mubarak alidhaniwa kupata mshtuko wa moyo alipohojiwa kwa mara ya kwanza mwezi Aprili.

Mubarak aliyekuwa rais, na kushikilia madaraka kwa miaka 30 na kuachia mwezi Februari baada ya wiki kadhaa za maandamano, kwa sasa anapata matibabu katika hospitali ya Sharm el-Sheikh akiwa chini ya ulinzi.

Pia anashutumiwa kuhusika katika mauaji ya waandamanaji waliopinga uongozi wake.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 83 ametiwa chini ya ulinzi kwenye hospitali tangu kuanza kupata matatizo ya moyo. Kizuizi chake kimeongezwa kwa siku 15 siku ya Ijumaa.