West Ham kupata meneja mpya karibuni

West Ham ina matumaini itamteua meneja mpya katika muda wa wiki mbili au tatu zijazo baada ya kuachana na Avram Grant.

Haki miliki ya picha Other
Image caption Avram Grant

Klabu ya West Ham ilitangaza kumtimua Grant siku ya Jumapili baada ya kuchapwa mabao 3-2 dhidi ya Wigan, hali iliyosababisha wateremke daraja.

Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya England Steve McClaren ni mmoja kati ya makocha wanaopewa nafasi kubwa ya kurithi kazi ya Grant.

Kocha wa kikosi cha kwanza Kevin Keen ndiye atakamata hatamu kwa muda na yeye pamoja na meneja wa zamani wa Newcastle Chris Hughton wanapewa nafasi baada ya McClaren.

Wengine wanaotajwa huenda wakachukua nafasi ya umeneja wa West Ham ni pamoja na Neil Warnock meneja wa sasa QPR, meneja wa zamani wa Bolton, Newcastle na Blackburn Sam Allardyce na mlinzi wa zamani wa West Ham Slaven Bilic.

Grant alichukua nafasi ya Jose Mourinho kuwa meneja wa Chelsea mwezi wa Septemba mwaka 2007, na akatimuliwa baada ya kuifikisha timu hiyo katika fainali ya Ubingwa wa vilabu vya Ulaya, ambapo walifungwa kwa mikwaju ya penalti na Manchester United.

Mwezi wa Novemba mwaka 2009 alichukua nafasi ya kuifundisha Portsmouth, lakini pamoja na mzozo wa kifedha, hakuweza kuisaidia klabu hiyo kushuka daraja.

Wamiliki wa West Ham David Gold na David Sullivan walimchukua Grant mwenye umri wa miaka 56, wakiwa na matumaini angeweza kuijenga West Ham imara katika Ligi Kuu ya Soka ya England.

Waliweza kuwasajili nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani Thomas Hitzlsperger, Frederic Piquionne na Pablo Barrera.

Hali ya kukata tamaa nusu ya kwanza ya msimu, iliibua taarifa huenda Grant nafasi yake ingechukuliwa na Martin O'Neill, lakini Grant aliendelea na kazi yake na akaruhusiwa kuwachukua wachezaji wengine akiwemo Demba Ba, Robbie Keane, Wayne Bridge na Victor Obinna.

Na bahati ya klabu hiyo ilionekana kunawiri pale waliposhinda mechi tatu kati ya tano mwezi wa Februari na Machi, ikiwemo ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Liverpool.

Lakini kufungwa na Wigan ilikuwa ni mara ya sita kwao katika michezo saba ya ligi, na kuwaacha wakiwa pointi sita nyuma chini kabisa ya jedwali na uongozi wa klabu ukaonelea wakati sasa umefika wa kufanya mabadiliko