Mke wa Mubarak akabidhi mali zake Misri

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Hosni Mubarak na mkewe Suzanne

Mke wa rais aliyeondolewa madarakani wa Misri Hosni Mubarak, aliyekuwa akishikiliwa kwa makosa ya ulaji rushwa, ameachiwa kwa dhamana baada ya kukabidhi mali zake.

Maafisa walisema Suzanne Mubarak alikabidhi nyumba ya kifahari iliyopo kwenye kitongoji cha mjini Cairo na fedha zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 3 zilizoshikiliwa kwenye akaunti mbalimbali za benki nchini Misri.

Familia ya Bw Mubarak inakabiliwa na madai ya "kupata mali kinyume cha sheria" wakati alipokuwa madarakani kwa miaka 30.

Bw Mubarak aliyeondoshwa madarakani mwezi Februari pia anashutumiwa kuhusika katika mauaji ya waandamanaji waliopinga uongozi wake.

Watoto wake wawili wa kiume, Alaa na Gamal, kwa sasa wanashikiliwa kwenye gereza la Tora kwa makosa ya udanganyifu.