Waziri wa mafuta wa Libya 'asaliti'

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Bw Shukri Ghanem

Waziri wa mafuta wa Libya Shukri Ghanem ameondoka nchini, huku kukiwa na ripoti kuwa ameisaliti serikali yake.

Maafisa wa Tunisia walisema Bw Ghanem- aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Libya- aliingia Tunisia kwa njia ya barabara kabla ya kwenda kwenye kisiwa cha Djerba.

Msemaji wa waasi wa Libya aliiambia BBC waziri huyo ameisaliti serikali yake, na alikuwa akielekea nchi moja iliyopo barani Ulaya.

Serikali ya Libya imesema alikuwa kwenye safari ya kikazi Tunisia, lakini Tripoli imesema wamepoteza mawasiliano.

Mwandishi wa BBC Andrew North, mjini Tripoli, alisema kama usaliti wa Bw Ghanem ukithibitishwa, atakuwa ni kiongozi wa daraja ya juu kuondoka tangu waziri wa mambo ya nje wa Libya Moussa Koussa kukimbilia Uingereza mwezi Machi.

" Shukri Ghanem ameondoka Libya," ofisa wa Tunisia ameliambia shirika la habari la AFP. Afisa huyo ameongeza Bw Ghanem alikwenda kwenye hoteli kisiwani Djerba lakini " hakujaribu kuwasiliana na serikali ya Tunisia".

Msemaji wa baraza la taifa la mpito la waasi lililopo Uingereza, Jumaa el Gamaty, aliiambia BBC: "Bw Shukri Ghanem amesaliti. Nadhani tunavyozungumza sasa yupo katika nchi ya mpito barani Ulaya."

Msemaji wa serikali ya Libya Moussa Ibrahim alisema Tripoli ilipoteza naye mawasiliano.