Mancini asema Tevez atabakia Man City

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini amesema nahodha Carlos Tevez anataka kuendelea kubakia katika klabu hiyo baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Stoke katika mchezo wa Ligi Kuu ya soka ya England.

Haki miliki ya picha 1
Image caption Carlos Tevez

Mustakabali wa mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina ulikuwa katika hali ya wasiwasi tangu alipowasilisha barua ya kutaka kuhama klabu hiyo mwezi wa Januari.

"Anao mkataba wa miaka mitano na ametuambia anataka kubakia," amesema Mancini baada ya kumshuhudia Tevez akifunga mabao mawili yaliyoinyanyua timu hiyo hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi.

Mancini ameongeza kueleza: "Aliwahi kusema hapo awali. Hana tatizo lolote."

Matamshi ya Mancini yanaonekana kupingana na yale yanayotoka kinywani mwa Tevez mwenyewe.

Mara tu baada ya kunyakua Kombe la FA siku ya Jumamosi kwa kuifunga Stoke bao 1-0, Tevez alisema "kuna jambo linalotakiwa kutafutiwa ufumbuzi na hili ni suala pana kulijadili kati yangu na familia yangu".

Na imekuwa ikifikiriwa kwa mapana kwamba Tevez atachagua kwenda kucheza soka Hispania ama Italia mwishoni mwa msimu.

Lakini kwa mujibu wa Mancini: "Nadhani atabakia hapa mwaka ujao. Hana tatizo lolote.

"Nimezungumza naye mara nyingi katika siku 20 zilizopita. Ni maoni yangu kwamba Carlos atabakia hapa masimu ujao.

"Mwezi wa Desemba alikuwa na tatizo. Lakini mtu yeyote anaweza kubadili mawazo yake.

"Carlos ni mchezaji muhimu hapa. Carlos ameshafunga mabao 20 msimu huu. Kila mara tumekuwa tukisema Carlos ni mchezaji muhimu. Carlos ni Carlos. Ni mshambuliaji mzuri sana na kwetu ni mchezaji murua. Anajisikia vizuri.