Ivory Coast yataka ICC ichunguze mauaji

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wakimbizi kutoka kabila la Guere

Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara ameiomba mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC kufanya uchunguzi wa madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu wakati wa ghasia zilizokuwepo nchini humo hivi karibuni.

Alisema sababu ya kuiomba mahakama hiyo ni " kutokana na mahakama za nchi hiyo kwa sasa haizna uwezo wa kusikiliza kesi nzito za uhalifu."

Takriban watu 3,000 waliuawa wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi zilizodumu kwa miezi minne.

Zaidi ya watu 25,000 bado wanaishi katika kanisa moja mjini Duekoue magharibi mwa nchi hiyo.

Walisema wanahofia maisha yao kwasababu wametoka katika kabila la Guere, ambao huonekana kumtii aliyekuwa rais Laurent Gbagbo, aliyekamatwa mwezi uliopita baada ya kukataa kushindwa katika uchaguzi wa mwaka jana.

Baada ya kuchukua madaraka, Bw Ouattara aliahidi uhalifu uliofanywa na pande zote wakati wa mgogoro nchini humo utafanyiwa uchunguzi.

Mwendesha mashtaka mkuu Luis Moreno-Ocampo tayari amesema ofisi yake inaandaa utaratibu wa kuchunguza madai ya mauaji ya watu wengi nchini Ivory Coast.