Rais wa Syria awekewa vikwazo

Rais Bashar el-Assad wa Syria Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Syria Bashar al-Assad

Marekani imemwekea vikwazo rais wa Syria Bashar al-Assad kwa tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu.

Hii ni mara ya kwanza kwa Bw Assad kulengwa moja kwa moja na jamii ya kimataifa kutokana na jinsi serikali yake inavyokabiliana na waandamanaji. Wengine waliowekewa vikwazo na Marekani ni maafisa 6 wa ngazi ya juu wa serikali ya Syria.

Mwezi uliopita Rais Barack Obama aliwawekea vikwazo kaka yake Mahir, binamu yake na mkuu wa idara ya ujasusi.

Taarifa kutoka serikali ya Marekani imesema wakati umewadia kwa Bw Assad ''Kuongoza siasa za kuleta mageuzi au aondoke''.

Wakati huo huo, Assad amesema vyombo vya usalama vilifanya makosa japo kidogo katika kukabiliana na maandamano hayo, gazeti la al-Watan limeripoti.

Aidha Assad ametoa hakikisho kuwa Syria imekabiliana na mzozo huo na kwamba maandamano yalikuwa yanamalizika sasa.

Maandamano nchini Syria yalianza mwezi Machi. Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani Bi. Hillary Clinton amesema watu wasiopungua elfu moja wameuawa katika makabiliano hayo na serikali.

Rais Assad sasa amewekwa kundi moja na kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi na Rais wa Belarus Alexander Lukashenko ambao pia wamewekewa vikwazo.