Mandela aenda kijijini kwake

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Bw Nelson Mandela na Bi Graca

Bw Nelson Mandela ameenda nyumbani kwake kijijini mjini Eastern Cape nchini Afrika kusini katika safari yake ya kwanza tangu alipolazwa hospitalini mwezi Januari.

Aliyekuwa rais wa nchi hiyo mwenye umri wa miaka 92 alitembelea Qunu akitokea mjini Johannesburg akiwa na kikosi cha madaktari.

Baada ya kuondoka uwanja wa ndege akisindikizwa na ujumbe wa magari 12, inasemwa yuko nyumbani kwake Qunu pamoja na mke wake.

Rais wa Afrika kusini Jacob Zuma alisema "amefurahi kwamba sasa afya yake imeimarika kiasi cha kuweza kusafiri".

Bw Mandela amekuwa akipata matibabu nyumbani kwake Johannesburg baada ya kutibiwa kutokana na matatizo ya moyo mapema mwaka huu.

Mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel hajatokea hadharani tangu sherehe za kufunga mashindano ya kombe la dunia mjini Johannesburg Julai 2010.