Ratko Mladic afikishwa mahakamani Belgrade.

Ratko Mladic. Haki miliki ya picha AP
Image caption Ratko Mladic.

Mahakama moja mjini Belgrade, imeahirisha kikao cha kwanza cha kusikilizwa kwa kesi ya kupelekwa hadi mahakama ya kimataifa ya kivita ICC mjini The Hague, mkuu wa zamani wa jeshi la Waserbia nchini Bosnia, Ratko Mladic aliyekamatwa siku ya Alhamisi baada ya kubaini kuwa hali yake ya kiafya ilikuwa mbaya.

Madaktari wataamua hivi leo ikiwa kikao hicho cha mahakama mjini Belgrade kitarejelewa au la.

Mladic alionekana kuwa hafifu na kuzongwa na uzee wakati akiingia katika mahakama moja mjini Belgrade akiwa amevalia kofia na koti nzito.

Punde baada ya kufika mahakani ambapo alitarajiwa kusomewa mashtaka dhidi yake, mara tu kesi ikaahirishwa.

Akizungumza na waandishi habari wakili wa Mladic, Milos Saljic alisema mjeta wake ana matatizo ya kiafya na alikuwa na matatizo ya kuzungumza.

Utawala wa Serbia uko maakini kuona Ratko Mladic anakabidhiwa mbele ya mahakama ya kimataifa ya jinai kwa haraka, kwa matumaini kwamba kuhamishwa kwake kutadidimiza maandamano kutoka wazalendo wa Kiserbia ambao wanamuona Generali huyo wa zamani kama mtetezi wa jamii ya wa-Serbia.

Image caption Washukiwa wengine wa mauaji ya Kimbari nchini Bosnia.

Hata hivyo kuna wengine ambao wamekaribisha kumatwa kwa Mladic, kwani hii inaondoa kikwazo kikubwa zaidi dhidi ya matumaini ya Serbia kujiunga na Muungano wa Ulaya.

Ratco Mladic alituhumiwa kwa uhalifu wa kivita hapo mwaka 1995 na mahakama ya kimataifa ya jinai iliyoko the Hague ambapo amelaumiwa kutekeleza mauaji ya kimbari.

Wakili wake hata hivyo anasema hatambui uhalali wa mahakama hiyo ya ICC.

Huku kukamatwa kwa mladic kukivutia hisia tofauti nchini Serbia, kimataifa hatua hiyo imepokelewa kwa sifa kuu.

Rais Barack Obama amempongeza mwenzake wa Serbia Boris Tadic, kwa juhudi zake kumsaka jenerali huyo wa zamani.

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron wamesema matukio ya sasa ni onyo kwa wahalifu wa kivita kwamba hatimae watakabiliwa na mkono wa sheria.