West Brom yafungua mazungumzo na Ode

West Brom inajiandaa kwa mazungumzo na mshambuliaji wake Peter Odemwingie kuhusiana na mkataba mpya, hii imethibitishwa na wakala wake.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Peter Odemwingie

Odemwingie mchezaji wa kimataifa wa Nigeria mwenye umri wa miaka 29, msimu huu uliomalizika alikuwa mfungaji bora wa klabu hiyo akiwa amefunga mabao 15 katika msimu wake wa kwanza tu wa kucheza Ligi Kuu ya soak ya England.

Odemwingie amefanya kazi kubwa kuiwezesha klabu hiyo kuwa nafasi za juu alipofunga katika michezo mitano mfululizo mwezi wa Aprili na Mei.

Mshambuliaji huyo amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake wa sasa pamoja na miezi mingine 12 ya kuchagua, lakini West Brom inakusudia kumzawadia mkataba mnono kutokana na jitahada zake.

Wakala wake David Omigie amesema anasubiri kwa hamu kusikia kutoka klabu hiyo hivi karibuni ili mazungumzo yaanze.