Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Shusha dereva

Bwana mmoja nchini Uchina alipatwa na hasira na kuamua kumshusha dereva wa gari la wagonjwa na kuendesha yeye mwenyewe baada ya kuona dereva huyo anaendesha kwa polepole.

Gazeti la Changjiang Daily limesema bwana huyo alikuwa anampeleka mke wake hospitali. Bwana huyo aitwaye Lin, aliita gari la wagonjwa baada ya kumkuta mkewe akiwa hajitambui kutokana na kunywa sumu baada ya wawili hao kugombana. Baada ya Lin kumpeleka katika zahanati, waganga wa hapo wakamshauri ampeleke mkewe katika hiospitali kubwa ya jimbo. Bwana Lin na mkewe wakaingia kwenye gari la wagonjwa kuelekea katika hospitali kubwa.

Hata hivyo wakiwa njia bwana Lin akawa anlalamika kuhusu mwedo wa taratibu, lakini dereva hakuwa akimsikiliza. Walipofika kwenye taa za barabarani na gari kusimama, katika eneo la Wuhan, bwana Lin alimvamia dereva huyo na kumtupa nje ya gari, na yeye mwenyewe kuanza kuendesha, moja kwa moja hadi hospitali, ambapo mkewe huyo alipelekwa katika wodi ya wagonjwa mahututi ICU.

Dereva wa gari la wagonjwa, yaani ambulace alikwenda kumshitaki bwana LIn polisi. Hata hivyo polisi waligoma kuchukua hatua zozote za kisheria, kwa sababu walimuonea huruma bwana Lin.

Baa gerezani

Mamlaka katika gereza moja nchini Mexico wamekuta wafungwa wamefungua baa ndani ya gereza.

Mtandao wa China Daily umesema katika baa hiyo wamekuta vinywaji vikali, bia na hata meza ya kuchezea pool. Polisi wa Ciudad Juarez waligundua baa hiyo siku ya jumatatu katika gereza hilo lililopo katika jimbo la kaskazini la Chihuahua, imesema taarifa kutoka ofisi ya mwendesha mashitaka mkuu.

Walikamata chupa ishirini za vodka, chupa ishirini za tequila na makopo mia mbili ya bia. Polisi pia walikuta bunduki tatu, simu 20 za mkononi, bangi misokoto mia moja na themanini na dozi tisini za dawa za kulevya aina ya heroin. Mkuu wa gereza hilo alifukuzwa kazi siku ya Jumatano, na maafisa wengine wa magereza wanachunguzwa, amesema Jorge Chaires, msemaji wa mwendesha mashitaka wa serikali kwa magereza.

Simu na mshale

Polisi nchini Marekani wamemkamata msichana mmoja kwa tuhuma za kumchoma na mshale baba yake.

Mtandao wa msnbc umesema baba huyo alikuwa amemnyanganya mwanaye huyo wa kike simu yake ya mkononi. Kachero wa polisi William Adam amesema baba huyo alichomwa na mwanaye mwenye umri wa miaka 15, kwa kutumia mshale wa kuwindia siku ya Jumatano.

Baada ya kuchomwa na mshale huo, baba huyo alilazimika kutambaa hadi nyumba ya jirani ili kuomba msaada, kwani binti yake huyo alimzuia asitumie simu ili kuomba msaada, kimeripoti kituo cha TV cha KOMO.

Bwana huyo alipelekwa hospitali na hali yake imeelezwa kuwa mbaya. Binti huyo alikimbilia katika msitu ulio karibu huku akiwa na mishale yake mingine iliyosalia. Hata hivyo polisi walimzingira na kumkamata, na anafanyiwa uchunguzi.

Mama na mwana

Mama mmoja na mwanae wa kiume wamesimamishwa kazi baada ya kudaiwa kuanzisha vurugu katika baa moja nchini, Marekani.

Mama huyo na mwanaye, wote ni polisi wa jiji la New Orleans. Mama huyo, Emelda Blanco na mwanaye Gerald walisimamishwa kazi siku ya Jumatano baada ya tuhuma kuwa walianzisha fujo na kupigana katika baa moja mjini humo.

Mtandao wa cnews.com umesema mama huyo amefanya kazi ya polisi kwa miaka ishirini na mitano, huku mwanaye huyo akiwa polisi kwa miaka mitatu.

Taarifa zinasema wawili hao walianzisha mtafaruku katika baa iitwayo Robertson Vieux Carre lounge na hata kupigana na mlinzi wa baa hiyo. mama huyo na mwanaye wamekamatwa na kushitakiwa kwa kosa la kufanya ugomvi mdogo.

Mtihani na muziki

Mwanafunzi mmoja wa kike huko Scotland ameruhusiwa kufanya mitihani huku akisikiliza muziki anaoupenda.

Msichana huyo alitishia kuichukulia hatua za kisheria shule yake iwapo wangemkatalia kusikiliza muziki wakati akifanya mitihani yake.

Waalimu awali walikataa ombi la mwanafunzi huyo, kwa kuogopa kuwa wanafunzi wengine nao wangetaka kufanya hivyo.

Wazazi wa mtoto huyo walikwenda katika mamlaka za shule ya Scotland kuwasilisha ombi la mtoto wao, lakini ombi hilo lilitupiliwa mbali.

Hata hivyo mamlaka hiyo ililazimika kubadili mawazo baada ya wazazi hao kusema watachukua hatua za kisheria. Walisema wangetumia kifungu cha haki sawa, wakidai mtoto wao huyo ana ugonjwa wa kutotulia na kusikiliza walimu akiwa darasani.

Mamlaka za Scotland zimekubali ombi hilo lakini zimewataka walimu kuhakikisha nyimbo anazosikiliza hazina majibu ya mitihani anayofanya.

Kafa, kazinduka

Familia moja nchini India iliyokuwa ikiomboleza kifo cha ndugu yao, ilipatwa na mshangao na hali ya furaha baada ya ndugu yao huyo kuzinduka.

Mke wa bwana huyo pamoja na jamaa zake walikuwa wakibubujikwa na machozi kwa kifo cha ghafla cha Vijay Kumar Ratre mwenye umri wa miaka 32, ambaye alikutwa akielea katika dimwi la maji kwa muda mrefu.

Mtandao wa Indo Asia news umesema polisi wa eneo hilo la Raipur walifika na kuuopoa mwili wa bwana huyo, huku kundi la karibu watu mia moja likiwa limekusanyika kuomboleza. Polisi waliita gari la kubebea wagonjwa ili mwili ufanyiwe uchunguzi kabla ya kwenda kuzikwa.

Mara tu mwili huo ulipowekwa ndani ya gari, bwana Vijay alizinduka na kujaribu kuruka na kutoka ndani ya gari. Umati wa watu uliokusanyika ulilipuka kwa furaha baada ya kuona tukio hilo. Polisi wamesema bwana huyo alikuwa amelewa chakari bila hata kujua kilichokuwa kikitokea.

Na kwa taarifa yako.....

Paka ana misuli thelatini na mbili katika kila sikio lake

Tukutane wiki ijayo... Panapo Majaaliwa