Rais Goodluck Jonathan aapishwa Nigeria

Viongozi wa Afrika na maelfu ya watu maarufu walihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, katika medani ya mji mkuu, Abuja.

Image caption Rais Goodluck Jonathan

Sherehe zilianza kwa wimbo wa taifa na kulikuwa na ulinzi wa hali ya juu.

Maombi yaliendeshwa na wakuu wa dini za Kiislamu na Kikristo nchini humo.

Uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita ulikumbwa na vifo vya mamia ya raia, katika ghasia zilizoibuka, ingawaje wengi wanasema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.

Bw Jonathan alishika hatamu ya uongozi baada ya Umaru Yar-Adua kufariki dunia takriban mwaka moja uliopita.

Rais Jonathan, maarufu kwa kofia yake kubwa, na kuupenda mtandao wa intaneti wa facebook, ameorodhesha majukumu mengi ya kutimiza, na wengi wataona amejipa kibarua kigumu, kama ataweza kuyatekeleza.

Muhimu zaidi ni kurejesha huduma ya umeme, na kuondosha rushwa.

Uchaguzi huo ulileta wasiwasi baina ya pande za kaskazini na kusini mwa Nigeria.

Rais Goodluck Jonathan anakabiliwa na jukumu la kuonesha kuwa hana mapendeleo.