Boko Haram: Tulitekeleza shambulio Nigeria

Polisi nchini Nigeria
Image caption Polisi nchini Nigeria

Wapiganaji wa kundi la kiislamu nchini Nigeria, Boko Haram wameiambia BBC kuwa walihusika na msururu wa mashambulio ya bomu baada ya kuapishwa rasmi kwa Rais Goodluck Jonathan siku ya Jumapili.

Shambulio hatari zaidi ni lile lililotokea katika kambi ya jeshi,mji wa kaskazini mwa Nigeria wa Bauchi ambako karibu watu 14 walifariki dunia.

Msemaji wa kundi hilo pia alisema walihusika na mauaji ya kaka yake kiongozi wa kidini wa Borno, mmoja wa viongozi muhimu wa dini ya kiislamu nchini Nigeria.

Kundi hilo limetekeleza mauaji kadhaa siku za hivi karibuni katika jimbo la Borno.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais wa Nigeria

Wanampinga mfumo wa elimu wa kimagharibi na kushtumu serikali ya Nigeria kwa kuendesha shughuli zake kwa misingi ya kimagharibi.

Mapigano katika mji mkuu wa jimbo la Borno, Maiduguri,kati ya Boko Haram na polisi mwezi Julai mwaka 2009 yalisababisha mauaji ya mamia ya watu,wengi wao wakiwa wa kundi hilo.

Kwa miezi minane iliopita,wapiganaji wa kundi hilo wamekuwa wakipigana vita vya kuvizia katika jimbo la Borno,wakiua polisi na watu wanaoamini wanasaidia maafisa wa usalama kuwakabili wao.