Uganda yatishia kuondoa majeshi yake Somalia

Rais wa Uganda Yoweri Museveni Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni, amesema kuwa serikali ya mpito ya Somalia inahitaji mwaka mmoja zaidi ili kukabiliana vyema na wapiganaji wa Kiislamu.

Alionya kuwa kama hilo halitazingatiwa, basi Uganda itaondoa vikosi vyake vinavyosaidia serikali ya mpito dhidi ya wapiganaji wa al-Shabab, alisema.

Muda wa sasa wa serikali hio inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa unamalizika tarehe 20 mwezi Agosti mwaka huu na Umoja wa Mataifa unataka uchaguzi ufanyike haraka.

Bwana Museveni amesema uchaguzi ukifanyika mwaka huu utatoa fursa kwa makundi ya wapiganaji kujipanga upya.

Uganda ina wanajeshi 5,000 katika kikosi cha muungano wa Afrika wanaolinda amani, nchini Somalia.

Burundi nayo inachangia idadi ilobakia.

" Inaonekana kwetu itakuwa bora kwa pande zote kama serikali ya mpito itaongezewa muda usiozidi mwaka mmoja," Bwana Museveni aliwaambia wajumbe wa mkutano wa kimataifa kuhusu Somalia mjini Kampala, Uganda.

Haki miliki ya picha other
Image caption Rais wa Somalia

Uchaguzi ukifanywa mapema,alionya, " Itakuwa ni nafasi kwa watu wenye misimamo mikali kujipanga upya na kuleta matatizo na kutia dosari mafanikio yote yaliyopatikana kufikia sasa".

Aliongeza: "kama utawala wa sasa utaondoka, au kama utadhoofishwa, basi itakuwa hatuna sababu ya kuendelea kukaa katika mazingira hayo - tutaondoka Somalia."

Rais wa Somalia Sharif Sheikh Ahmad aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa hali kwa sasa nchini humo si shwari kwa kufanya uchaguzi. Hata yeye alitaka muda wa serikali ya mpito uongezwe.