Ethiopia yajitolea wanajeshi Sudan

Ethiopia imejitolea kupeleka wanajeshi wa kulinda amani nchini Sudan katika mpaka wenye mzozo katika eneo la Abiyei, baada ya wanajeshi wa upande wa kaskazini kudhibiti eneo hilo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Eneo la Abiyei

Wachambuzi wameonesha wasiwasi kuwa mzozo wa Abiyei huenda ukazusha vita mpya ya wenyewe kwa wenyewe kati ya Sudan kaskazini na kusini ambayo inatarajia kuanza kujitawala mwezi Julai.

Maafisa wa upande wa kusini wamekubali hatua hiyo ya Ethiopia, lakini upande wa kaskazini bado unatafakari jambo hilo.

Hatua hii imekuja baada ya pande hizo mbili kukubaliana kuweka eneo lililo huru kijeshi katika mpaka na kufanya doria kwa pamoja.

Mtaalam wa masuala ya Sudan Alex De Waal, ambaye amekuwa akifanya kazi na mazungumzo ya upatanishi chini ya Umoja wa Afrika, ameiambia BBC kuwa majadiliano ya jinsi ya mpango huo utakavyotekelezwa bado yanaendelea.

Takriban watu milioni moja na nusu walikufa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya kaskazini na kusini vilivyodumu kwa miaka 22 na kumalizika mwaka 2005.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililaani udhibiti wa Abiyei na kutoa wito wa kuondolewa kwa haraka kwa wanajeshi wa kaskazini katika eneo ilo lenye utajiri wa mafuta ambalo upande wa kusini pia unadai ni lake. Lakini balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa Daffa-Alla Elhag Ali Osman amesema watatekeleza hilo wakati makubaliano mapya ya kisiasa na kuisalama yatakapofikiwa.

Wakati huohuo, amesema serikali ya Sudan inataka wanajeshi wa kulinda amani waondoke wakati Sudan Kusini itakapokuwa huru mwezi Julai.