Nato yaongeza mda wake Libya

Shirika la Nato limejiongezea kipindi cha kuendesha shughuli zake nchini Libya kwa siku 90 zaidi.

Uwamuzi huo ulikubalika moja kwa moja na Mabalozi kutoka nchi 28 wanachama wa shirika hilo kwenye mkutano wao mjini Brussels.

Shirika la NATO linaipiga Libya chini ya kivuli cha kunusuru maisha ya raia wa nchi hiyo wanaohujumiwa na utawala wa Kanali Ghaddafi.

Haki miliki ya picha
Image caption shambulio la ndege za Nato huko Libya

Shughuli nzima huko Libya iliidhinishwa na Umoja wa Mataifa tarehe 31 March na kuongozwa na Ufaransa, Uingereza na Marekani na mda wake ulitazamiwa kumalizika tarehe 27 Juni mwaka huu.

Mbali na wanachama wa Nato, mazungumzo hayo kwenye makao makuu ya shirika hilo yalishiriki pia wana balozi za nchi ambazo si wanachama wa Nato ikiwa ni; Jordan, Qatar, Sweden, United Arab Emirates na Morocco.

Majeruhi

Uwamuzi ulikuwa wa kutimiza wajibu wa kuwashirikisha waratibu wa kijeshi kutoka nchi zinazochangia vikosi.

Lakini wandishi wa habari wanasema kuwa uwamuzi huo pia ulikusudia kuwapelekea risala raia wa Libya ambao kwa kipindi cha miezi mitatu wamejitahidi kumpindua Kanali Muammar Gaddafi baada ya kuwaongoza kwa zaidi ya miaka arobaini.

Katibu mkuu Nato, Anders Fogh Rasmussen ameuambia mkutano wa wandishi habari kuwa ''Suali siyo kama Gaddafi ataondoka au lini. Huenda akapinduliwa baada ya mda mrefu au hata kesho.

Wakosoaji wa mpango wa Nato nchini Libya wanasema umekwama.

Baadhi ya waliokubaliana na mpango huo wakati wa kura katika baraza la usalama -hususan Urusi wanashangazwa kuona kwamba mpango uliokusudia kuwalinda raia dhidi ya vikosi vya Kanali Gaddafi sasa umegeuka kuwa wa kuindua serikali nzima.

Mamlaka ya Libya yanadai kuwa ukweli wa mambo ni kwamba mbali na kuwalinda raia mashambulio ya Nato yameuwa hadi raia 700, ingawa Nato inakanusha madai hayo.