Mjane wa Sisulu A Kusini afariki dunia

Haki miliki ya picha AP
Image caption Bw Nelson Mandela na Bi Albertina Sisulu mwaka 2005

Afrika Kusini inaomboleza kifo cha mmoja wa watu walioongoza harakati za kupambana na ubaguzi wa rangi, Albertina Sisulu, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 92.

Bi Sisulu alikuwa mjane wa Walter Sisulu, rafiki na mshauri wa aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela.

Mwanasiasa mashuhuri wa aina yake, alikuwa mpambanaji katika shirikisho la wanawake wa African National Congress (ANC)

Msemaji wa ANC Brian Sokutu alisema Bi Sisulu alikuwa wakati wote wa maisha yake akiwa katika harakati za kuleta demokrasia nchini Afrika Kusini.

Gazeti la Afrika Kusini la South Africa Times limemnukuu akisema, " Komredi Sisulu ametumia muda wake wote kuitumikia ANC na kuikomboa Afrika Kusini. Tunatoa heshima zetu kwa kiongozi huyu na mama wa harakati hizi."

'Hakuwahi kukata tamaa'

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Bi Albertina Sisulu na mumewe Walter Sisulu

Viongozi mashuhuri kutoka chama tawala cha ANC wamekuwa wakitembelea nyumbani kwa familia ya Bi Sisulu kaskazini mwa Johannesburg kutoa heshima zao za mwisho.

Ahmed Kathrada, rafiki wa muda mrefu, alisema alimchukulia Bi Sisulu kama mama na alishtushwa sana na taarifa ya kifo chake.

Bw Kathrada alinukuliwa akisema, " Kisiasa alikuwa mtetezi wa haki za binadamu, komredi mzuri, rafiki mpendwa na ni mwenye mvuto. Hakukata tamaa.

Taarifa za kifo chake zilipotolewa Alhamis jioni, mitandao ya kijamii Afrika Kusini ilifurika watu wakitoa heshima zao za mwisho, kwa aliyekuwa akijulikana kama "Ma Sisulu"

Bi Sisulu alikutana na Walter Sisulu katika miaka ya 40 baada ya kuhamia Johannesburg kufanya kazi kama muuguzi.

Japo hakutoka kwenye familia ya kisiasa, alijijenga haraka kama mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi kwa namna yake na ni miongoni mwa walioongoza maandamano mwaka 1956 ya wanawake 20,000 kupinga kulazimishwa kutumia kitambulisho.

Wakati mumewe alipokuwa gerezani na Bw Mandela, alijikuta akipewa kifungo cha nyumbani mara kwa mara.

Hata hivyo, alikuja kuwa mjumbe wa ANC, akitembelea viongozi nchi za nje na kufahamisha watu juu ya harakati za kupambana na ubaguzi wa rangi.

Mwaka 1994 alichaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia wa Afrika Kusini.

Alikuwa mmoja miongoni mwa watu pekee walioruhusiwa kukaa pembeni ya Bw Mandela, alipoumwa na kulazwa hospitali mapema mwaka huu.