Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Tangazo la kazi

Image caption Kitanzi

Kama uko tayari kufanya kazi yoyote mahala popote -- kuna kazi imetangazwa -- huko India vijijini -- kazi ya kunyonga watu.

Maafisa wa gereza la Jorhat, karibu maili mia mbili mashariki mwa Gauhati, wanatafuta mtu atakayekuwa tayari kupeleka watu kwenye kinyongeo.

Majaji nchini India aghalabu hutoa hukumu za kifo. Gazeti la Metro limesema watu wawili tu wamenyongwa nchini humo katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Myongaji mwenye uzoefu nchini humo Nata Mullick alikufa mwaka 2009.

Bwana Mullick ambaye mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka themanini na nne, na akiwa tayari amestaafu, alilazimika kuitwa kwa dharura ili kumnyonga mtu aliyekuwa amehukumiwa kifo wakati huo.

Wafanyakazi katika magereza ya karibu na Jorhat, katika majimbo ya Uttar Pradesh na West Bengal wameulizwa iwapo wanaitaka kazi hiyo, lakini hakuna mtu aliyejitokeza mpaka sasa.

Iwapo hakuna mtu atapatikana kufanya kazi hiyo, huenda hukumu za kifo zilizotolewa zikawa mashakani. Kuna watu watau kwa sasa ambao wamehukumiwa kunyongwa nchini India.

Panya mla nguruwe

Mfugaji mmoja nchini Australia hakuamini macho yake alipokuta mifugo yake ikishambuliwa na panya.

Mfugaji huyo wa kusini mwa Australia John Gregory aliingia katika banda lake la kufugia nguruwe na kukuta nguruwe wake mmoja akiliwa na mamia ya panya waliomvamia, umeripoti mtandao wa news.com.

"Tatizo la panya limekuwa kubwa mno" amesema bwana Gregory. Katika kukabiliana na nguruwe wake kutafunwa na panya, mfugaji huyo ameamua kuwapaka nguruwe wake mafuta machafu ya engine-- maarufu kama oili chafu.

"Hawa panya wameishiwa chakula, wanawaparamia nguruwe na kuwatafuna" amesema Gregory na kuongeza "Lakini hawapendi ladha ya mafuta machafu na ndio salama yangu" amesema mfugaji huyo.

Amesema sumu ya panya inauzwa bei ghali na hivyo analazimika kutumia njia kama hizo za ujanja. "Sisi wakulima tunapenda vitu vya bei nafuu" amesema Gregory "Wakati mwingine huwa nachanganya sukari na simenti, panya wanapenda sukari, wakiila, ile simenti inaganda tumboni mwao" amesema Gregory.

Panya ndani ya ndege

Shirika la ndege za Australia lililazimika kufuta safari yake moja, baada ya wafanyakazi wa ndege kukuta vitoto vitano vya panya ndani ya ndege.

Panya hao waligundiliwa muda mfupi tu kabla ya abiria kuanza kuingia ndani ya ndege kuanza safari mjini Sydney. Panya hao walikutwa katika moja ya kabati ndogo ndani ya ndege hiyo aina ya Boeng 767.

Msemaji wa shirika hilo amesema panya hao walikamatwa na kuuawa, na ndege hiyo kusimamisha safari zake kwa muda wa saa thelathini na sita. Shirika hilo limesema hili ni jambo lisilo la kawaida, na kuwa hakuna dalili yoyote ya uharibifu ambayo umefanywa.

Figo kwa iPad

Kijana mmoja nchini Uchina alikuwa akitamani sana kupata kifaa kipya cha mawasiliano aina ya iPad 2 kiasi kwamba aliamua kuuza figo yake ili anunue kifaa hicho.

iPad ni kifaa cha kisasa ambacho kinaweza kufanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuhifadhi muziki na pia kurambaza kwenye mtandao.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 17 aliyejulikana kwa jina moja tu la Zheng alikiri kwa mama yake kuwa aliamua kuuza figo yake baada ya kuona tangazo la mtu anayetaka kununua figo kwa dola elfu mbli za kimarekani.

"Nilitamani sana kuwa na iPad 2 lakini sikuwa na pesa" amesema kijana Zhang akizungumza na kituo cha televisheni cha Shenzen, katika jimbo la Guangdong. Kijana Zheng aliporudi nyumbani mama yake aligundua mara moja.

"Aliporudi, alikuwa na laptop mpya na iPad mpya" amesema mama yake, huku akionesha kidonda ambapo mwanae alifanyiwa upasuaji kutoa figo. "Nilitaka kujua alipata wapi pesa za kununua vitu hivyo vya gharama kubwa, na ndipo akakiri kuwa ameuza figo yake moja" amesema mama huyo.

Simu za iPhone na kifaa cha iPad ambazo hutengenezwa na kampuni ya Apple ni maarufu sana hasa kwa vijana kuonesha ufahari wao nchini Uchina.

Jamaa kakatwa nanihii

Mwanamama mmoja nchini Bangladeshi ameukata--- CUT--- uume wa mwanaume mmoja-- SHOUT-- na kuupeleka polisi kama ushahidi kuwa alikuwa akitaka kubakwa. Kwa mujibu wa mtandao wa BBC mwanamama huyo mwenye umri wa miaka arobaini alifanya hivyo siku ya Jumatatu.

Mwanamama huyo ambaye ameolewa na ana watoto watatu, amedai kuwa alishambuliwa wakati akiwa amelala katika wilaya ya Jhalakathi, karibu kilomita mia mbili kusini mwa mji mkuu Dhaka.

Maafisa wa polisi wanasema mwanaume anayetuhumiwa kutaka kumbaka pia ana miaka arobaini na ana watoto watano. "Wakati akijaribu kumbaka, mwanamke huyo alimkata kwa kutumia kisu, halafu akaifunga kwenye mfuko wa karatasi na kuileta polisi kama ushahidi" amesema Abdul Khaer, mkuu wa polisi wa huko.

Kipande hicho kilichokatwa kiliachwa polisi wakati mshukiwa huyo akitibiwa hospitali. Hata hivyo mtuhumiwa huyo anasema mwanamama huyo alikuwa mpenzi wake, na alimtaka watoroke wakaishi pamoja.

Bwana huyo amesema alipokataa ombi la mwanamke huyo, ndipo alishambuliwa. Mkuu wa polisi Khaer amesema watamkamata, mara tu atakapopata nafuu. Daktari wa hospitali anapotibiwa mtuhumiwa huyo amesema imeshindikana kuunganisha kipande kilichokatwa.

Na kwa taarifa yako

... Ukifika umri wa miaka 75, utakuwa umelala kwa takriban miaka 23 kwa jumla...

Tukutane wiki ijayo.... panapo majaaliwa