Uingereza ina watoto wengi maskini

Image caption Umaskini Uingereza

Japokuwa Uingereza ni miongoni mwa nchi tajiri duniani, bado inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizoendelea zenye idadi kubwa ya watoto maskini.

Karibu mtoto mmoja kati ya kila watoto watatu anaishi katika familia zinazopokea chini ya asilimia 60 ya pato la wastani nchini Uingereza.

Ripoti ya shirika la watoto la 'Save The Children' imesema watoto milioni 1.6 wameathiriwa na umaskini kiasi kwamba hawapati chakula cha kutosha au wanaishi katika makazi yenye baridi na yenye nafasi ndogo.

Kila serikali mpya ikija inaahidi kuimarisha viwango vya maisha kwa watoto lakini hilo linashindikana.

'Save The Children Fund' linasema moja kati ya sababu nyingi ni kuwa sauti ya watoto walio maskini zaidi haisikiki kabisa.

Baada ya shirika hilo kutoa nafasi kwa watoto kujieleza, baadhi walilalamika kuwa wakati mwingine wanakosa mlo wa jioni.

Wengine wakazungumzia kukosa mahali pa kuchezea , kunyanyaswa shuleni wanapokuwa hawana mavazi mapya au kuonekana wachafu.

Ripoti hiyo iliyoitwa 'eleza wazi kama ilivyo' inafuatia utafiti wa hivi karibuni kutoka Shirika la Kimataifa la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo- OECD, ilionyesha kuwa watoto nchini Uingereza wanashindwa kuepuka hali za ufukara zaidi kuliko nchi nyingine yoyote tajiri.

Mazungumzo kati ya 'Save The Children' na baadhi ya watoto pia yatarushwa katika kipindi cha runinga cha BBC kitakachoonyeshwa England na Scotland.

Idadi ya watoto wanaoishi katika umaskini nchini Uingereza imepungua kwa kiasi cha watoto milioni moja katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Hata hivyo 'Save The Children Fund' linataka serikali ya Uingereza pamoja na wanasiasa kuchukua hatua zaidi katika kazi zao kuwakumbuka watoto walio katika mazingira magumu.

Sally Copley kutoka shirika hilo ameeleza kuwa fedha zaidi zinahitajika kuwekezwa katika elimu kusaidia watoto walio maskini zaidi kupata ajira bora na hali bora za maisha ya baadaye kuliko wazazi wao.

Mwezi Aprili serikali ya Uingereza ilitangaza mkakati wa kumaliza umaskini unaowakabili watoto kufikia mwaka 2020.

Iliahidi kuwasaidia wazazi ambao hawana ajira kwa kuondoa vikwazo vinavyowasababishia hali hiyo , kutoa huduma bora za jamii kwa kwa familia na kuwasaidia watoto walio katika hali duni na za ufukara.