NATO imeshambulia makaazi Tripoli

NATO inasema inachunguza madai ya wakuu wa Libya, kwamba ilipiga mabomu kwenye eneo la makaazi ya mji mkuu, Tripoli.

Haki miliki ya picha AP

Mwandishi wa BBC anasema alipopelekwa kwenye tukio, aliona nyumba ya ghorofa tatu iliyoangamia na miili mwili ikitolewa hapo. Jeremy Bowen akiwa Tripoli anasema:

"Tulipowasili kwenye mtaa tuliona waokozi na watu wa mtaani wakichimba kifusi mara nyingi kwa mikono tu, kutafuta walionusurika.

Jengo liloshambuliwa liko mtaa wa Souk al Juma, eneo la makaazi, kama maili moja kutoka uwanja wa ndege wa jeshi, ambao umeshawahi kushambuliwa na NATO mara kadha.

Majirani wanasema shambulio lilitokea kama saa saba za usiku. Nyumba iliyoangamia ilikuwa ya familia moja.

Ilionesha ilishambuliwa kwa ndege au kombora.

Jukumu la NATO ni kuwalinda raia.

Ikiwa hili ni shambulio lilofanywa na NATO, basi kutazuka maswala kuuliza, jee NATO inafanya nini Libya na inapata mafanikio gani?

Swala hilo piya litaulizwa na baadhi ya wanachama wa NATO ambao tangu awali, hawakuridhia operesheni ya kijeshi.

Tukio hilo la Tripoli, linafuatia shambulio jengine lilofanywa na NATO karibu na mji wa mafuta wa BREGA siku ya Alkhamisi, ambalo liliuwa wapiganaji.

NATO iliomba msamaha kwa makosa hayo."