UN inataka msaada uruhusiwe Abyei

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa taarifa kulaani kitendo cha serikali ya Sudan kuuteka mji wenye mzozo, wa Abyei, na kutaka wanajeshi waondoshwe huko.

Haki miliki ya picha BBC World Service

Jeshi la Sudan, lilivamia eneo hilo baina ya mpaka wa Sudan Kaskazini na Kusini, na kufanya wakaazi maelfu kadha kukimbia.

Mbali ya kulaani kutekwa kwa Abyei na jeshi la Khartoum, taarifa piya inatoa wito kwa pande zote mbili kuruhusu msaada upelekwe kwa wale walioathirika na mapigano, na wakaazi waliohama waruhusiwe kurudi.

Maelfu ya wakaazi wa Abyei walikimbilia kusini, jeshi la serikali ya Sudan lilipouteka mji na kuuchoma moto na kupora mali.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wana wasi-wasi kuwa mapigano ya kuania Abyei, yanaweza kuzusha mapambano makubwa zaidi baina ya Kaskazini na Kusini, kabla ya uhuru wa Sudan Kusini tarehe 9 July.

Taarifa hiyo piya inalaani shambulio lilofanywa na Sudan Kusini dhidi ya askari wa Umoja wa Mataifa, waliokuwa wakiwasindikiza wanajeshi wa Kaskazini.

Serikali ya Sudan inasema hiyo ndiyo sababu ya kuchukua hatua ya kijeshi.

Baraza la Usalama linataka pande zote mbili zikubali jeshi la Umoja wa Mataifa libaki Abyei.