Lengo jipya kuhusu UKIMWI

Miaka 30 tangu ugonjwa wa UKIMWI kutambulikana, viongozi wanaokutana katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wameamua kuhakikisha kuwa watu milioni 15 wenye UKIMWI wawe wanapata matibabu, ufikapo mwaka wa 2015.

Hiyo ni zaidi ya mara dufu ya idadi inayopata dawa hivi sasa.

Hatua zilizokubiliwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa watoto wote watazaliwa bila ya kuambukizwa UKIMWI, ufikapo wakati huo wa mwaka 2015.

Lakini mkutano haukutoa ahadi ya kuzidisha fedha za kutekeleza lengo hilo.

Mshauri wa Shirikala la madaktari wanaojitolea, Doctors without Borders - Sharonann Lynch - anasema azimio hilo litawasaidia wale wenye UKIMWI:

"Wagonjwa wa UKIMWI wakisikia azimio hili, watasema: 'vema, serikali yangu imeahidi kuhakikisha kuwa watu wote wenye virusi vya HIV, watakuwa wanapata dawa ufikapo mwaka wa 2015.'

Na hilo ni jambo ambalo sisi sote, lazima tuchagize serikali kutekeleza."