Gharama za chanjo kupungua

Dawa
Image caption Chanjo kupungua bei

Kampuni kadhaa za kutengeneza dawa zimetangaza kupunguza bei za chanjo muhimu za magonjwa katika mataifa yanayoendelea.

Chanjo hizo zilizopunguzwa bei zinanuiwa kukinga na kutibu magonjwa ya kuhara na kupatika, kichomi , kifua kikuu na magonjwa mengine.

Mpango huo utasaidia shirika la kimataifa linalohusika na chanjo za tiba na elimu ya kukinga maradhi GAVI kufikia malengo yake, ya kutoa dawa kwa mamilioni ya watoto wanaokabiliwa na tisho la kuangamia kutokana na maradhi.

Malengo ya Milenia

Moja ya malengo ya milenia ya Umoja wa Mataifa, ni kupunguza vifo vya watoto wadogo kwa asilimia 60 ifikiapo mwaka wa 2015.

Lakini hii itategemea kujitolea kwa shirika la kimataifa, GAVI, linalohusika na kutoa chanjo na elimu ya kukinga maradhi kwa watoto milioni ishirini na nne kote duniani ambao hawajapata chanjo yoyote.

Faida

Inakadiriwa kuwa watoto milioni 9 walio na umri wa chini ya miaka mitano hufa kila mwaka kutokana na magonjwa ambayo yangezuiwa kwa kutumia Chanjo.

Gharama ya juu ya chanjo hiyo ni kizingiti kikubwa katika harakati za kutibu magonjwa hayo, na shirika la Gavi amabalo pia hushughulika na kununua dawa zitakazo tumika katika mataifa masikini, linakabiliwa na upungufu wa karibu dola bilioni 4

Na tangazo la kutoka kwa kampuni za kutengeneza dawa kuwa zitapunguza bei ya chanjo hiyo kwa hadi asilimia 75 kwa mataifa yanayostawi ni afueni kwa shirika hilo.