Mbowe kufikishwa mahakamani Arusha

Dk Freeman Mbowe Haki miliki ya picha ippmedia
Image caption Kiongozi wa upinzani TZ, dkt Freeman Mbowe

Kiongozi Mkuu wa upinzani nchini Tanzania, Dk Freeman Mbowe, anatarajiwa kufikishwa mbele ya Mahakama moja ya mkoa wa Arusha, Kaskazini mwa nchi hiyo.

Bw Mbowe alikamatwa na polisi hapo jana kwa madai ya kukiuka sheria za dhamana.

Kukamatwa kwa Bw Mbowe kunakuja siku chache baada ya mahakama moja mjini Arusha kuamuru akamatwe baada ya kukiuka dhamana.

Anashutumiwa kwa kutojitokeza kortini wakati wa kesi inayomkabili pamoja na viongozi wenzake wa Chama Cha Demokrasia (CHADEMA), ya madai ya kuandaa mkutano na kuandamana kinyume cha sheria, Januari 2011.

Hata hivyo kukamatwa kwa Dk Mbowe kumesababisha hisia kali. Mbunge wa CHADEMA John Mnyika, ametaja kukamatwa kwake kama udhalalishaji. ''Ni shambulio dhidi ya bunge na shambulio dhidi ya wabunge'', Bw Mnyika amesema.

Naye mwenyekiti wa cha chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, anadai kukamatwa kwa kiongozi wa upinzani bungeni ni njama ya kudhoofisha kambi ya upinzani bungeni, katika kipindi hiki cha kutayarisha bajeti ya nchi.