Marekani yathibitisha kifo cha Fazul

Waziri wa mashauri ya nje wa Marekani Bi Hillary Clinton, amesema kifo cha Fazul Abdullah Mohammed, aliyeshukiwa kuwa mkuu wa Al Qaeda Afrika Mashariki, "ni pigo kubwa" kwa kundi hilo na washirika wake.

Jumamosi serikali ya Marekani imethibitisha kifo cha Fazul Abdullah Mohammed, katika tukio la kufyatuliana risasi na vikosi vya Somalia mjini Mogadishu.

"Kifo cha Harun Fazul ni pigo kubwa kwa Al Qaeda, washirika wake wa siasa kali, na shughuli zake Afrika Mashariki," Clinton aliwaeleza waandishi wa habari akiwa mjini Dar es Salaam, Tanzania.

"Ni mwisho unaostahili kwa gaidi aliyewaletea wengi kifo na huzuni watu wasiokuwa na hatia Nairobi, Dar es Salaam na kwingineko; Watanzania, Wakenya, Wasomali na wafanyakazi wetu wa ubalozi".

Awali afisa mmoja wa cheo cha juu katika serikali ya Marekani alithibitisha kifo cha kiongozi huyo wa Al Qaeda Afrika Mashariki, na kuipongeza serikali ya muda nchini Somalia.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Alishukiwa kuhusika na milipuko ya balozi za Marekani katika miji ya Nairobi na Dar es Salaam

Kiongozi huyo wa Al Qaeda katika kanda ya Afrika ya Mashariki Fazul Abdullah Mohammed, alishukiwa kuhusika na shambulio dhidi ya balozi za Marekani katika Kenya na Tanzania mnamo mwaka 1998.

Fazul Abdullah amekuwa mtu anayetafutwa sana barani Afrika baada ya zaidi ya watu 220 kuuawa na zaidi ya 5000 kujeruhiwa katika mashambuliio ya mwaka 1998.

FBI iliahidi dola milioni 5 kwa kichwa chake

'Pasi ya Kigeni' Maafisa wa usalama wa nchini Somalia wameyaambia mashirika ya habari ya AFP na Reuters kuwa Fazul Abdullah na mwenzake waliuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa serikali ya mpito ya Somalia katika kizuizi cha barabarani siku ya Jumatano.

"Vikosi vyetu viliwafyatulia risasi wawili hao waliokataa kusimama katika kizuizi cha barabarani. Walijaribu kujitetea walipozingirwa na askari wetu," kamanda wa majeshi ya serikali ya mpito ya Somalia Abdikarim Yusuf ameliambia shirika la habari la AFP.

"Tulichukua vitambulisho vyao mkiwemo pasi ya kigeni pamoja na dawa, simu za mkononi na komputa za laptop," akaongeza.

Duru za maafisa wa Somalia zimeifahamisha AFP kwamba Fazul alikuwa amebeba kiasi cha dola elfu 40,000 taslimu na pasi ya kusafiria ya Afrika Kusini ikiwa na jina "Daniel Robinson".

Pasi hiyo ilitolewa Aprili 13, 2009, ikionyesha kwamba aliondoka Afrika Kusini Machi 19, 2011 kuelekea Tanzania, ambako alipewa kibali cha kuingia.

Afisa mwaandamizi wa usalama nchini Somalia Halima Aden, amethibitisha kuwa Fazul aliuawa katika kizuizi cha barabarani, wiki hii na kwamba alikuwa na pasi ya Afrika Kusini.

"Baada uchunguzi tulithibitisha kuwa ni yeye na tukamzika," aliliambia shirika la habari la Reuters.

Mkuu wa polisi wa Kenya , Matthew Iteere, amewaambia waandishi habari mnamo siku ya Jumamosi kwamba anashauriana na maafisa wa Somalia kupata ripoti kamili.

"Tumeambiwa kulikuwa na magaidi wawili waliouwawa nchini Somalia mnamo siku ya Jumaatano. Walitajwa kuwa ni Fazul Mohammed na Ali Dere. Hayo ndio tulioelezwa na wenzetu," aliviambia vyombo vya habari nchini Kenya.

Hata hivyo msemaji wa vikosi vvya kulinda amani vya Muungano wa Afrika nchini Somalia amesema picha za maiti hazielekei kuwa zinafanana na Fazul Abdullah Mohammed.

Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Al Shabab limesema taarifa za kuuawa kwake si kweli.

Fazul Abdullah alizaliwa katika visiwa vya Comoro katika miaka ya 1970, na inaaminiwa alijiunga na kundi la al-Qaeda nchini Afghanistan katika miaka ya 1990.

Baada ya mashambulio ya balozi za Marekani katika miji ya Nairobi na Dar es Salaam, Tanzania, mwaka 1998, ambapo watu 224 waliuwawa; Marekani ilimshtumu kwa kuhusika na kutoa tuzo za dolla milioni 5 kwa mtu yeyote atakayetoa habari zitakazosababisha kukamatwa kwake.

Mnamo mwaka 2002, Abdullah pia alishtumiwa kwa kuhusika na mashambulio dhidi ya hoteli ya Kikambala mjini Mombasa, Kenya na jaribio la kuidungua ndege ya shirika la Israel.

Mwaka 2007, alinusurika shambulio la ndege za kivita za Marekani katika kijiji cha Haya, kusini mwa Somalia, karibu na mji wa Ras Kamboni.