Serikali yawaadhibu watu Jisr Al-Shughur

Waandamanaji nchini Syria Haki miliki ya picha AP
Image caption Waandamanaji nchini Syria

Ripoti kutoka Syria zinasema kuwa serikali inawaadhibu watu wanaoishi katika mji wa kaskazini ambako inasema wanajeshi 120 waliuwawa na magenge ya watu waliojihami mapema wiki hii.

Wakaazi wa mji wa Jisr Al-Shughur, ambao BBC iliwasiliana nao wanasema wagonjwa wamenyimwa matibabu katika hosipitali za serikali, na wanafunzi kutoka mji huo wamezuiliwa kufanya mitihani.

Ripoti hizo zinadai wanajeshi wa Syria wakiwa na magari ya kivita wameuzingira mji huo.

UN yaishutumu Syria

Wakati huo huo, kamishna wa Umoja wa mataifa kuhusu haki za kibinadamu Navi Pillay ameishutumu Syria kwa kupiga vita wananchi wake.

Katika taarifa yenye maneno makali aliyotoa mjini Geneva, amesema kuwa Syria inazima maandamano kwa kutumia ukatili na makabiliano makali.

Amesema kuwa zaidi ya watu elfu moja wameuawawa na maelfu ya wengine kutiwa mbaroni tangu machafuko hayo yaanze mapema mwezi machi.

''nimefuatilia kile kinachoendelea katika eneo lote hilo na nimejionea uhasama mbaya sana. kile tunachokiona sasa ni kuwa Syria imekiuka maadili yote. Nimeona kuwa lazima nizungumze na kushutumu mauaji yanayofanyika. '' Navi Pillay amesema.