Gavana wa Israel kuwania cheo cha IMF

Gavana wa benki ya Israel, Stanley Fischer, alitangaza siku ya Jumamosi kwamba naye ameamua kuwania madaraka ya kuliongoza shirika la fedha ulimwenguni, IMF.

Kuna uwezekano mkubwa sasa ushindani utakuwa mkali mno kati yake na Christine Lagarde kutoka Ufaransa, na ambaye ilielekea alikuwa anaongoza katika kampeni ya kuitafuta kazi hiyo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Stanley Fischer katika picha ya pili ya juu kuanzia kushoto

"Kulijitokeza nafasi nzuri, na pasipo kupanga, na ambayo huenda isijitokeze tena, katika kuwania nafasi ya kuiongoza IMF, na baada ya kufikiria kwa muda mrefu, nimeamua kulizingatia jambo hilo", Fischer alieleza katika taarifa yake.

"Haya ni licha ya utaratibu mgumu, na vikwazo ambavyo huenda vikajitokeza," alielezea.

Fischer, mwenye umri wa miaka 67, anatazamiwa huenda akawa ni mpinzani mkali wa waziri wa fedha wa Ufaransa, Christine Lagarde.

Katika kura ya maoni iliyoendeshwa na Reuters miongoni mwa wanauchumi, na iliyochapishwa mwezi Mei, kati ya wahusika 56, 32 walimuunga mkono Lagarde, na ambaye pia wengi katika muungano wa Ulaya wa EU wanadhani atafaa kuyasimamia madaraka hayo.

Fischer, wakati mmoja alikuwa ni naibu wa mkurugenzi mkuu wa IMF.

Anasifiwa na wengi kwa kuusaidia uchumi wa Israel kustawi, hasa kwa kupunguza viwango vya riba mapema mwaka 2008.

Tangu wakati huo, ameinua viwango hivyo mara kumi, katika jitihada za kuzuia kuporomoka kwa bei na mapata, na kuuwezesha uchumi kuendelea kustawi kwa asilimia 5 mwaka huu wa 2011.