Albertina Sisulu azikwa

Sala ya maziko ya Albertina Sisulu, mfuasi mashuhuri wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, imehudhuriwa na watu wengi Soweto pamoja na watu mashuhuri wa nchi hiyo.

Haki miliki ya picha BBC World Service

Rais Zuma alitaka Bibi Sisulu apewe mazishi ya kitaifa.

Majenerali walibeba jeneza la Bibi Sisulu katika ibada hiyo iliyofanywa kwenye uwanja mkubwa wa michezo wa Soweto, ambako Rais Jacob Zuma aliongoza maombolezi.

Alisema: "Enzi imemalizika, na taifa limeondokewa; lakini tuna fahari kwamba tukimjua Mama Albertina Sisulu.

Tunamzika shujaa na mama wa taifa. ambaye alikuwa jabari na imara katika kupambana na ukandamizi wa ubaguzi wa rangi, huku akiwa na huruma kwa maskini na wanyonge.

Hapo awali, Nelson Mandela alisema Bibi Albertina Sisulu alikuwa mmoja kati ya wazalendo wakubwa wa Afrika Kusini.

Bwana Mandela alikuwa mpambe kwenye harusi ya Bi Albertina na hayati Walter Sisulu - ambaye alimshawishi Mandela ajiunge na chama cha ANC.