Mazishi ya Wanjiru yafanyika

Samuel Wanjiru Haki miliki ya picha AFP
Image caption Amezikwa Jumamosi mjini Nyahururu

Maelfu ya waombolezaji wamehudhuria mazishi ya bingwa wa Olimpiki wa mbio za marathon Jumamosi, Sammy Wanjiru, aliyefariki mnamo mwezi uliopita baada ya kuanguka kutoka roshani ya nyumba yake.

Mazishi yalifanyika katika uwanja wa michezo katika wilaya alikozaliwa, Nyahururu, katika jimbo la Rift Valley.

Mahakama iliamuru wiki hii kuwa Wanjiru, aliyekuwa na umri wa miaka 24, anaweza kuzikwa licha ya kuwa uchunguzi unaendelea kuhusu mazingira yaliyosababisha kifo chake.

Polisi wamesema kuwa Wanjiru alikufa ama katika ajali, au alijiua baada ya mkewe kumfumania na mwanamke nwengine.

Mamaake Wanjiru, Hannah, hakuhudhuria mazishi hayo. Wanjiru alikuwa Mkenya wa kwanza kushinda medali ya dhahabu ya Olimpiki katika mbio za marathon za michezo ya Beijing mnamo mwaka 2008 na akihesabiwa kuwa mojawapo wa vijana chipukizi hodari.

Aliheshimiwa kwa kupigiwa saluti ya mizinga 21 wakati jeneza lake lilipoteremshwa kaburini katika shamba lake. Mazishi yake yalihudhuriwa na wanariadha mashuhuri wa Kenya mkiwemo anayeshikilia rekodi ya dunia katika mbio za mita elfu tatu Daniel Komen, aliyekua bingwa wa dunia wa mbio za marathon Catherine Ndereba, na aliyekuwa bingwa wa dunia katika mbio za masafa ya mita elfu tano, Benjamin Limo. David Beckford, mkurugenzi wa mbio za marathon za jiji la London, aliwaambia waombolezi katika mazishi hayo kuwa Wanjiru alikuwa ni mojawapo wa wakimbiaji hodari kabisa wa mbio za marathon duniani licha ya umri wake mdogo na kwamba sifa zake zinaweza kulinganishwa na mkimbiaji mashuhuri wa Ethiopia Haile Gebreselassie.