Matokeo ya Kombe la Shirikisho - Afrika

Klabu ya Asec Mimosas ya Ivory Coast na InterClube ya Angola ni miongoni mwa vilabu ambavyo vimefuzu kwa raundi ya makundi mashindano ya kuwania kombe la shirikisho barani Afrika.

Haki miliki ya picha supersport
Image caption Naodha wa Sofapaka akimkabili mchezaji wa Club African katika uwanja wa Nyayo mjini Nairobi

InterClube ambayo kwa wakati mmoja ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-0 dhidi ya Difaa el-Jadida ya Morocco, ilitoka sare ya kufungana mabao 2-2, na kufuzu kwa raundi ijayo.

Mjini Nairobi, klabu ya Sofapaka imeyaaga mashindano hayo licha ya kuilaza Club Africain kwa mabao 3-1 katika mechi hiyochezwa katika uwanja wa taifa wa Nyayo.

Sofapaka ilihitaji kufunga mabao 4-0 baada ya kulazwa mabao 3-0 katika mechi yao ya raundi ya kwanza mjini Tunis.

Nahodha wa Sofapaka James Situma amesema licha ya kuondolewa kwao, timu hiyo ilicheza mchezo mzuri lakini bahati haikuwa yao.

Mabingwa wa zamani wa kombe hilo Asec nayo ilitoka sare ya 1-1 na Primeiro kutoka Angola na kufuzu kwa raundi ijayo kwa jumla ya mabao 5-1.

Klabu ya Moghreb Fes kutoka Morocco pia imefuzu kwa raundi hiyo ya makundi baada ya kuilaza Zesco kutoka Zambia mabao 2-0.

Katika matokeo mengine, mabingwa wa zamani wa kombe la klabu bingwa barani Afrika, JS Kabylie ya Algeria, iliilaza Diaraf kutoka Senegal mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa mjini Tizi-Ouzou na kufuzu kwa michuano ya robo fainali.

Timu hizo mbili zilitoka sare ya kutofungana bao lolote katika mechi ya raundi ya kwanza.