Ujerumani yawatambua waasi wa Libya

Waziri Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waziri Westerwelle

Ujerumani imetambua waasi wa Libya kama "Wawakilishi halali wa wananchi wa Libya".

"Tunataka Libya huru, ya amani na demokrasia bila ya kuwepo Muammar Gaddafi," Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema katika ngome ya waasi mjini Benghazi.

Takriban mataifa kumi na mbili yametambua Baraza la mpito la Taifa.

Ujerumani ilishutumiwa kwa kukataa kuunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, la kuruhusu majeshi ya Nato kulinda raia wa Libya.

Baraza hilo la mpito liliundwa na majeshi yaliyoanzisha upinzani dhidi ya utawala wa Kanali Gaddafi, Februari 16.

Baada ya miezi ya mapigano makali, Kanali Gaddafi amesalia na udhibiti wa mji mkuu Tripoli, huku waasi wakishikilia mji wa Benghazi na eneo kubwa la mashariki.

Akizungumza kwa pamoja na waziri wa mambo ya nje wa waasi, Ali Issawi, Bw Westerwelle amesema: "Tuna lengo moja: Libya bila Gaddafi.

"Baraza la taifa ndio wawakilishi halali wa watu wa Libya."

Wananchi wa Libya waliokuwa wakisikiliza, walipiga kofi baada ya tangazo hilo.

Afisa wa ngazi ya juu, makamu mwenyekiti wa baraza, Abdel Hafez Ghoga, amefurahishwa na uamuzi huo wa Ujerumani akisema ni "Hatua kubwa sana".

Wanasdiasa wa upinzani, wanahabari na wataalam wa sera za nje wa Ujerumani, walishutumu serikali kwa kutojiunga na mashambulizi ya Nato, na kuituhumu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kimataifa.