Fedha zaidi kugharamia chanjo

David Cameron Haki miliki ya picha AP
Image caption Ametoa ahadi ya Uingereza kutoa msaada zaidi katika kampeni ya kutoa chanjo kote duniani

Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, ametoa ahadi ya kutoa pauni milioni 814, zitakazotumiwa katika kuwapa watoto chanjo kote duniani, katika kuzuia magonjwa yanayoweza kukomeshwa kama vile yale ya pumu na kuharisha, ambayo husababisha vifo vya watoto wengi katika mataifa yanayoendelea.

Alitoa ahadi hizo katika mkutano wa kimataifa mjini London, baada ya kuulizwa kuongezea pauni bilioni 2.3 kufikia mwaka 2015, katika kugharamia chanjo kwa watoto.

Shirika la dunia linalohusika na utaratibu wa kutoa chanjo, Global Alliance on Vaccines and Immunisation, limesema hatua hiyo itaweza kuokoa maisha ya watu milioni nne katika kipindi cha miaka minne.

Serikali ya Uingereza tayari imepanga kutumia fedha zaidi kuliko taifa lolote lile, kiwango cha dola bilioni 2 katika kipindi cha miaka 30.

Kiwango hicho cha pesa pauni milioni 814 ni juu ya kile cha sasa ambacho Uingereza inaendelea kutoa, cha pauni milioni 680, kutolewa kati ya mwaka 2011 hadi 2015.

Akishirikiana na Bw Cameron kama mwenyeji wa mkutano, tajiri wa kampuni ya Microsoft, Bill Gates, amesema atatoa dola bilioni moja katika kuisaidia kampeni hiyo ya chanjo.

Inatazamiwa kwamba kufikia mwisho wa mkutano, kuna uwezekano wa fedha kuzidi kiwango kinachotazamiwa, cha pauni bilioni 2.3.

Mbali na Uingereza, mataifa mengine yaliyotoa ahadi za kuongeza fedha kwa kampeni hiyo ni pamoja na Australia.

Image caption Rais wa Liberia amesema chanjo imebadilisha maisha ya wengi duniani

Akiwahutubia wajumbe, rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, amesema chanjo kwa watoto husaidia sana katika kuyabadilisha maisha ya watu.

"Chanjo kwa watoto huyafanya maisha kuwa tofauti kabisa. Ni tofauti kubwa. Mataifa 63 yameandikisha chanjo kuwafikia watu asilimia 90. Mataifa kumi kusini mwa Sahara yamo katika nchi kumi za mwanzo zinazowafikiwa wengi kwa huduma hii," alielezea Sirleaf.

Bi Sirleaf alielezea kwamba huduma hiyo inaweza kuwafikia wengi zaidi kwa wahisani "kuongeza kiwango cha msaada wao, kupunguzwa kwa bei za chanjo, na kuongezwa kwa ushirikiano wa kifedha kwa mataifa yanayoendelea, na yanayonufaika kutokana na mpango wenyewe".