Maelfu ya watu wahama Kordofan Kusini

Wakimbizi Kordofan Kusini Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mashirika ya misaada yazuiwa kuwasaidia walioathirika na vita

Zaidi ya watu elfu hamsini wamelazimika kuhama makaazi yao katika jimbo la kordofan kusini kufuatia mashambulizi ya anga kutoka jeshi la Sudan.

Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, limesema mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu pia yamezuia kuwasaidia watu walioathirika kufuatia mashambulizi hayo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Fatoumata Lejeune-Kaba ameelezea kuwa makundi ya wapiganaji yameweka vizuizi barabarani na yanawazuia kupeleka misaada kwa watu waliohama makaazi yao.

Na Mkuu wa kanisa la Kianglikana, Askofu Rowan Williams amesema kuwa huenda hali katika jimbo la Kordofan Kusini ikazidi kuzorota sawa na hali ilivyo katika jimbo la Darfur.

Mzozo huo unaingia siku ya kumi sasa.

Inaripotiwa kuwa mapigano yamekuwa makali kati ya vikosi vya serikali na wanajeshi wa zamani wa jeshi la Kusini.

Sudan Kusini imebakisha siku kadhaa kabla nchi hiyo kubwa barani Afrika haijagawanywa.

Mwandishi wa BBC Peter Martell aliyeko mji mkuu Juba anasema ndege za jeshi la Sudan Kaskazini zimelipua eneo la kijeshi la anga lililoko Kauda katikati ya milima ya Nuba, kwenye makazi ya makundi yanayounga Sudan Kusini likiwaita waasi.

Umoja wa mataifa unaripoti kuwa milio mikubwa ya risasi iliweza kusikika huku mapigano yakisambaa katika jimbo la Kordonfan Kusini.

Kuna wasiwasi kuwa idadi ya watu waliokufa ikaongezeka, huku wafanyakazi wa misaada na viongozi wa dini katika eneo hilo wakisema kuwa wanaolengwa ni wale wanaoaminika kuipinga serikali ya Khartoum.

Watu wanachimba mahandaki wakiogopa mashambulizi zaidi.

Awali wafanyakazi wa misaada walisema mapigano yanazidi kuongezeka katika jimbo la Nuba, ambako ni makazi ya makabila ya waafrika ambao wana uhusiano zaidi na Sudan Kusini kuliko Kaskazini inayokaliwa na waarabu wengi.