Kesi ya aliyekuwa Rais wa Tunisia kuanza

Waandamanaji nchini Tunisia Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais Ben Ali alazimika kuondoka madarakani kufuatia maandamano

Kesi ya aliyekuwa rais wa Tunisia Zine al-Abidine Ben Ali, itaanza tarehe 20 Juni, licha ya kuwa hatakuwepo.

Ben Ali alitorokea Saudi Arabia mnamo mwezi wa Januari.

Akitangaza tarehe ya kesi hiyo, waziri mkuu wa muda wa Tunisia Beji Caid Essebsi amesema Saudi Arabia bado haijasema ikiwa itamrejesha Ben Ali nchini humo.

Rais huyo wa zamani anakabiliwa na mashtaka ya ulanguzi wa madawa ya kulevya na kupanga njama dhidi ya serikali ya Tunisia.

Lakini wakili wa Ben Ali amepuuza msingi wa kesi hiyo. Rais huyo wa zamani na mke wake, Leila Trabelsi, wanakabiliwa na mashtaka.

Kujiuzulu kwake mamlakani, kuliwapa moyo waandamanaji katika nchi za kiarabu, kutoka Misri hadi Yemen kupinga utawala dhalimu katika nchi hizo.

Kesi hiyo itafanywa katika mahakama ya kijeshi na ya kiraia. Serikali ya Tunisia imesema mashtaka ya kwanza yatashughulikia kupatikana kwa fedha, dawa za kulevya na silaha katika makazi ya rais huyo wa zamani.

Kulingana na shirika la habari la AFP, takriban kilo mbili za dawa za kulevya na dola milioni 27 za Marekani zilipatikana kwenye nyumba yake. Kiongozi huyo pia anakabiliwa na mashtaka ya mauaji na ubadhirifu wa fedha.