Gen.Nyamwasa atishiwa kufukuzwa

Mashirika yanayopigania haki za binadamu nchini Afrika ya kusini yamechukuwa hatua za kisheria kuitaka serikali ya nchi hiyo ibadili hadhi ya ukimbizi aliyopewa mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda.

Image caption Lt.Gen Kayumba Nyamwasa

Wamesema kuwa serikali ilichukuwa hatua ya haraka kumpa hifadhi Luteni Generali Faustin Kayumba Nyamwasa il hali alishirikiana na Rais Paul Kagame katika kukomesha mauwaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Lakini akakimbilia nchini Afrika ya kusini mwaka jana baada ya kukorofishana na Bw.Paul Kagame.

Yeye anatakikana na Uhispania pamoja na Ufaransa kwa madai ya mchango wake katika mauwaji ya kimbari ya siku 100.

Baada ya kukimbilia Afrika ya kusini aliponea chupuchupu jaribio la kumua.Serikali ya Rwanda ilikanusha madai ya kwamba ilihusika katika jaribio hilo.

Afrika ya kusini ilimwitisha balozi wake aliyekueko mjini Kigali baada ya tukio hilo.

Hukumu akiwa uhamishoni

Uhispania na Ufaransa zinamsaka Lt Gen Nyamwasa, kwa tuhuma za kuongoza mauwaji ya Rais wa zamani wa nchi hiyo Juvenal Habyarimana, tukio lililoanzisha mauwaji ya kimbari.

Shirika lijulikanalo kama 'The Southern Africa Litigation Centre and the Consortium for Refugees and Migrant Rights' limesema kuwa haikubaliki kwa Afrika ya kusini kuruhusu mtu wa aina hiyo kupewa hadhi ya ukimbizi akiwa anashukiwa kushiriki vitendo vinavyokiuka haki za binadamu.

"sheria ya ukimbizi ina lengo la kuwalinda wanyonge, na siyo wale waliosababisha uonevu na kusababisha wengi kuingia katika hali kama hiyo, alisema Allan Wallis, wakili kwenye kituo cha Afrika kusini (The Southern Africa Litigation Centre.)

Serikali ya Rwanda nayo imekuwa ikiipa msukumo Afrika ya kusini imrejeshe Rwanda Lt Gen Nyamwasa atumikie kifungo gerezani cha miaka 24 kufuatia mahakama ya kijeshji kusikiliza na kumhukumu mnamo mwezi januari kwa tuhuma za kutishia usalama wa taifa, kukimbia jeshini bila ruhusa na uchafuzi wa jina la taifa.

Image caption Watu 800,000 waliuawa

Takriban watu wa kabila la Watutsi 800,000 pamoja na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa katika mauwaji hayo ya kimbari.

Bw.Kagame aliongoza vuguvugu la RPF ambalo lilikomesha mauwaji mnano mwaka 2000 na tangu hapo amekuwa ndiyo Rais wa nchi.

Baada ya mauwaji, aliahidi kuleta amani na utawala wa demokrasia lakini wakosoaji wanasema anaongoza utawala wa ki-imla.