Dembele kujiunga na SC Freiburg

Shambulizi matata wa Mali Garra Dembele amejiunga na klabu ya SC Freiburg inayoshiriki katika ligi kuu ya soka nchini Ujerumani, Bundesliga kutoka kwa klabu ya Levski Sofia ya Bulgaria.

Haki miliki ya picha eufa.com
Image caption Mshambulizi wa Mali Garra Dembele

vilabu vingi vilikuwa vikitaka kumsajili mchezaji huyo aliyeifungia klabu yake Levski jumla ya mabao 34 baada ya kucheza mechi 36 msimu uliopita.

"Dembele atajiunga na klabu yetu kuanzia siku ya Jumatatu ijayo'' afisa mkuu wa mawasiliano wa klabu hiyo Rudi Raschke alisema.

Hata hivyo Raschke, hajasema lolote kuhusu mkataba wa mchezaji huyo au kiasi cha fedha walichotumia kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25.

Mkurugenzi wa klabu hiyo, Dirk Dufner, amesema kusajiliwa kwa Dembele ni baraka kwa klabu hiyo hasa safu yake ya mashambulio.

Baadhi wanahisi kuwa mchezaji huyo raia wa Mali, huenda akachukua mahala pa Papiss Demba Cisse kutoka Senegal.

Haki miliki ya picha uefa.com
Image caption Garra Dembele

Cisse ambaye alifunga mabao 22 msimu uliopita, amehusishwa na vilabu kadhaa barani Ulaya.

Lakini klabu hiyo imesema haijapokea ombi kutoka kwa klabu yoyote inayotaka kumsajili Cisse, ambaye ameonyesha nia ya kuchezea klabu yoyote inayoshiriki kwenye ligi ya klabu bingwa barani Ulaya.

Mapema mwaka huu mahakama moja mjini Bulgaria, iliimpa Dembele kifungo cha nje cha miezi minane, baada ya kupatikana na hatia ya kuendesha gari akiwa mlevi na pia kuwa na leseni bandia ya kuendesha gari.

Mahakama hiyo pia ilimpiga marufuku ya kuendesha gari lolote katika mataifa yote ya muungano wa Ulaya kwa muda wa miezi 9 kufuatia kukamatwa kwake mwezi Desemba mwaka uliopita.