Ben Ali ahukumiwa kifungo cha miaka 35

Ben Ali Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Aliyekuwa rais wa Tunisia Ben Ali

Mahakama moja nchini Tunisia imemhukumu rais wa zamani Zine al-Abidine Ben Ali na mkewe Leila kifungo cha miaka 35 jela kwa ubadhirifu na utumiaji mbaya wa mali ya uma.

Wawili hao, ambao walikimbilia Saudi Arabia mwezi Januari baada ya mapinduzi ya kiraia, pia wametakiwa kulipa faini ya dola milioni $66m.

Kesi hio iliyofanywa siku moja pekee na bila washtakiwa kuwepo mahakamani iliangazia pesa na vito vya thamani vinavyosemekana kuwa dola milioni $27m na ambazo zilipatikana katika moja ya kasri zao.

Kesi ya pili inayomhusu Ben Ali peke yake, na hasa kuhusu kuwa na mihadarati na silaha,iliahirishwa.

Uchunguzi unaendelea

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mahakama ambayo kesi dhidi ya Ben ali ilisikilizwa

Wakili wa Ben Ali amesema kuwa hukumu hiyo ilitolewa kwa misingi ya kisiasa na "ni mzaha".

Mwandishi wa BBC Jon Leyne mjini Tunis, anasema kuwa si rahisi kwa Saudi Arabia kuruhusu wawili hao kurudishwa Tunisia.

Miezi mitano baada ya wao kulazimishwa kutoroka nchini, Ben Ali na Leila Trabelsi wamehukumiwa bila ya wao kuwepo katika mahakama ya uhalifu mjini Tunis.

Waendesha mashtaka wanasema pesa na vito vya thamani, vyengine vikiwa "vya kihistoria", vilipatikana kwenye kasri yao huko Sidi Bou Said, sehemu ilio nje ya mji mkuu.