Aliyekuwa makamu wa rais Uganda kortini

Aliekuwa makamu rais wa Uganda Prof Gilbert Bukenya anatazamiwa kufika mahakamani leo kujibu mashataka ya kutumia vibaya madaraka yake.

Uchunguzi unaonyesha kuwa serikali ya Uganda ilipoteza mabilioni ya pesa wakati wa maandalizi ya mkutano wa jumuiya ya madola mjini Kampala.

Haki miliki ya picha googleimages
Image caption Pesa zilizotumika vibaya zilinunua magari aina ya BMW yaliotumika kwenye mkutano huo

Prof. Bukenya, alikuwa makamu rais wa Uganda hadi Mei 23 mwaka huu alipovuliwa madaraka hayo na Rais Yoweri Museveni.

Spika wa zamani wa bunge Edward Ssekandi ndio aliyeteuliwa kuchukua nafasi yake.

Afisa mmoja wa idara ya ukaguzi wa serikali alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa serikali ya Uganda ilikuwa imeweka kando bajeti ya dola za kimarekani million 120 kwa maandalizi ya mkutano wa jumuiya ya madola uliofanyika Uganda mwaka wa 2007.

Hata hivyo pesa zinazosemekana kutumiwa ziliongezeka hadi kufikia dola million 217.

Katika bunge lililopita kamati ya bunge ya matumizi ya umma, ilifanya uchunguzi kuhusu matumizi ya pesa za kuandaa mkutano huo na miongoni mwa mengine tume hiyo ilipendekeza kuwa Prof Bukenya awajibike kutokana na hasara iliopataikana.

Prof Bukenya alikuwa mwenyekiti wa kamati andalizi ya mkutano wa CHOGM na anahusishwa na ugawaji wa tenda za kununua pikipiki pamoja na magari aina ya BMW yaliyotumiwa na wageni kwenye mkutano huo.

Pesa zinazokadiriwa kupotea katika ubadhilifu huo ni dola takriban million 100. Haijulikani ikiwa Prof Bukenya atahudhuria kutokana na taarifa katika vyombo vya habari nchini Uganda akinukuliwa kusema kuwa hajapewa barua ya kumuita mahakamani.