Biashara ya mihadarati imekithiri Afrika

Maafisa wa serikali ya Nigeria
Image caption Maafisa wa serikali ya Nigeria wakiteketeza madawa ya kulevya

Idara ya Umoja wa Mataifa inayokabiliana na mihadarati na uhalifu inasema juhudi za kunasa watu na mihadarati Afrika Magharibi zimepungua sana kutokana na walanguzi kutumia mbinu tofauti kupitisha madawa ya kulevya kama vile cocaine.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa na waakilishi wa serikali za Afrika Magharibi walikutana mjini Dakar,Senegal kujadili mbinu za kupambana na uhalifu huo.

Wahalifu bado wanaendelea kupitisha mihadarati katika mipaka ya Afrika Magharibi huku maafisa wa usalama wakijaribu kuzuia biashara inayokadiriwa kuwa na thamani ya dola za Marekani bilioni moja,kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Ni watu wachache kutoka Marekani ya Kusini ambao hutumia Afrika Magharibi kupitisha mihadarati lakini raia wengi wa eneo hilo wanaaminika kuhusika pia.

Sasa kuna magenge ya wahalifu wa madawa ya kulevya katika eneo hilo,na wamefanikiwa kuukwepa mtego wa maafisa wa kukabiliana na mihadarati na biashara na magendo.

Afisa wa Umoja wa Mataifa anasema kuwa hata kama hakuna ushahidi wa uhusiano wa magenge hayo na kundi la Al Qaeda la Afrika Magharibi,bila shaka wanatoa huduma nyengine ili wapate pesa za kuendesha shughuli zao.