27 waangamia katika mlipuko Afghanistan

Mlipuko mkubwa wa bomu ulitokea katika hospitali moja katika mkoa wa mashariki wa Afghanistan, Logar, na kati ya waliokufa ni wanawake, watoto na wakongwe.

Image caption Hospitali iliyoshambuliwa imo wilaya ya Azra

Afisa mkuu wa afya wa mkoa huo, ameielezea BBC kwamba watu wasipoungua 27 waliuawa na 53 kujeruhiwa.

Alielezea kuna uwezekano kwamba watu zaidi walikufa, kwani baadhi ya watu waliamua kuondoka na maiti za jamaa zao.

Hospitali hiyo iliharibiwa vibaya mno, na baadhi ya watu walifunikwa kwa vifusi.

Maafisa walililaumu kundi la Taliban kwa mlipuko huo katika wilaya ya Azra, lakini kundi hilo limekanusha kuhusika.

Msemaji wa Taliban amesema wao kwa kawaida hawana nia ya kuwashambulia raia, na kwamba "mtu aliyekuwa na ajenda" fulani ndiye aliyehusika.

Mwandishi wa BBC mjini Kabul, Bilal Sarwary, amesema kundi la Taliban siku zote hujiepusha kudai limehusika panapotokea mauaji ya raia wengi.

Imekuwa vigumu kuthibitisha idadi kamili ya vifo vilivyotokea Jumamosi kufuatia mlipuko huo.

Awali wizara ya afya ilitangaza kwamba watu 60 walikufa, na maafisa wa mtaa na wale wa serikali mjini Kabul walitangaza idadi tofauti.