Boko Haram ni kundi la aina gani?

Kundi la Kiislamu la Nigeria lenye silaha, Boko Haram, lilitangaza kwamba lilihusika katika mlipuko wa bomu katika makao makuu ya polisi mjini Abuja, Alhamisi iliyopita.

Limeelezea kwamba linafanya juhudi kuiondoa serikali ya Nigeria na kuanzisha taifa la Kiislamu.

Wafuasi wake inasemekana wanazingatia aya ya Kuran inayoelezea: "Yeyote anayeongozwa kwa njia tofauti kinyume na aliyoyafichua Allah ni miongoni mwa watenda dhambi".

Haki miliki ya picha nema
Image caption Watu sita walikufa wakati makao makuu ya polisi yaliposhambuliwa kwa bomu Abuja

Boko Haram huendeleza Uislamu ambao huonyesha ni "haram", au jambo ambalo limekatazwa, kwa Waislamu kuhusika katika shughuli zozote za kisiasa au kijamii ambazo zinaambatana na mifumo ya mataifa ya magharibi.

Hayo ni pamoja na shughuli za uchaguzi, kuvaa T-shati na suruali ndefu, au kupata elimu ya kisasa na isiyokuwa ya kidini.

Wafuasi wa Boko Haram wanaamini serikali ya Nigeria inaongozwa na watu wasiomwamini Mungu, hata nchi hiyo ilipoongozwa na rais Mwislamu.

Jina halisi la kundi hilo ni Jama'atu Ahlis Sunna Lidda'awati wal-Jihad, ambalo kwa Kiarabu linamaanisha "Watu wanaozingatia na kufanya jitihada za kusambaza mafundisho ya Mtume na Jihad."

Lakini wakaazi wa mji wa kaskazini-mashariki mwa Nigeria wa Maiduguri, ambako kundi hilo lina makao yake makuu, walilibandika kundi hilo jina Boko Haram.

Kwa tafsiri ya moja kwa moja katika lugha ya Kihausa, jina hilo linamaanisha elimu ya magharibi iliyokatazwa.

Neno boko asili yake ni bandia, lakini baadaye lilitumika kuzungumzia elimu ya magharibi, na haram ni jambo ambalo limekatazwa.

Tangu siku za uongozi wa Khalifa akiwa Sokoto, na uliohusika katika kuyatawala maeneo ya kaskazini ya Nigeria, Niger na kusini mwa Cameroon, maeneo hayo yalipotawaliwa na Waingereza kuanzia mwaka 2003, elimu ya magharibi ilipingwa sana na baadhi ya Waislamu katika maeneo hayo.

Familia nyingi za Waislamu hukataa kuwapeleka watoto wao katika shule zinazosimamiwa na serikali, zikielekea kuwa na mifumo ya magharibi, na tatizo hilo kuwa baya zaidi kwa kuwa viongozi wa maeneo hayo hawadhani elimu ni jambo muhimu.

Chini ya misingi kama hiyo, mfuasi wa dini ya Uislamu, Mohammed Yusuf, alianzisha kundi la Boko Haram katika mji wa Maiduguri mwaka 2002.

Alianzisha kituo kikubwa, na ambacho kilikuwa sio tu na msikiti, bali pia chuo cha Kiislamu.

Boko Haram huchukizwa na elimu ya magharibi, na wafuasi wake wangependelea sharia za Kiislamu kutumika.

Waislamu wengi, na kutoka familia maskini kutoka maeneo mengi ya Nigeria, na hata kutoka nchi jirani, waliwasajili watoto wao katika chuo hicho.

Lakini Boko Haram hawakuwa tu na nia ya kuhusika katika elimu.

Nia yao kisiasa ilikuwa ni kuanzisha taifa la Kiislamu, na chuo hicho kilitumiwa katika kuwasajili wapiganaji kupambana dhidi ya serikali.

Mwaka 2009, Boko Haram liliendesha mashambulio kadha dhidi ya vituo vya polisi na majengo mengine ya serikali mjini Maiduguri.

Kilichotokea ilikukwa ni hali ya kufyatuliana risasi katika barabara za Maiduguri.

Mamia ya wafuasi wa Boko Haram waliuawa, na mamia ya wakaazi wa Maiduguri waliukimbia mji huo.

Hatimaye vikosi vya usalama vya Nigeria viliyazingira makao makuu ya kundi hilo, na kiongozi wa kundi hilo, Yusuf, kuuawa.

Image caption Kiongozi wa Boko Haram Mohammed Yusuf aliuawa baada ya kukamatwa

Mwili wake ulionyeshwa katika runinga ya taifa, na vikosi vya usalama kutangaza huo ndio mwisho wa Boko Haram.

Lakini wapiganaji wake wamekusanyika tena, na chini ya kiongozi ambaye bado hajajulikana, mwaka jana walilishambulia gereza la Maiduguri, na kuwafungulia huru mamia ya wafungwa wanaoliunga mkono kundi hilo.

Mashambulio yake mengi hufanywa na waendeshaji pikipiki, ambao wamefanikiwa kuwaua maafisa wa poli, wanasiasa, na yeyote yule anayewapinga, ikiwa ni pamoja na viongozi wengine wa Kiislamu na hata mhubiri wa Kikristo.

Katika miezi ya hivi karibuni, kundi hilo limefanya mashambulio ya waziwazi kaskazini mwa Nigeria.

Kati ya mashambulio hayo ni mlipuko wa mwezi Desemba katika mji wa Jos, shambulio la siku kuu ya mwaka mpya katika kambi ya wanajeshi ya Abuja, na milipuko kadhaa wakati wa kuapishwa kwa rais Goodluck Jonathan mwezi Mei.

Sasa kundi hilo limeyashambulia makao makuu ya polisi, na kuthibitisha kwamba kundi lenyewe bado lipo.

Tisho hilo huenda likaendelea kwa muda, ikifikiriwa kwamba eneo hilo la kaskazini mwa Nigeria lina umaskini mkubwa, na makundi yenye misingi kama ya Boko Haram yamekuwepo kwa muda.

Wadadisi wa kisiasa wanasema tatizo hilo litakwisha tu ikiwa serikali ya Nigeria itajitahidi kupunguza umasiki mkubwa katika eneo hilo, na kuanzisha mfumo wa elimu ambao utawafurahisha Waislamu wengi katika maeneo hayo.