Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Osama kusakwa

Haki miliki ya picha AP
Image caption Osama Bin Laden

Mzamiaji mmoja wa Marekani, anajiandaa kwenda katika bahari ya Uarabuni, na kupiga mbizi kuusaka mwili wa Osama Bin Laden

Mzamiaji huyo, Bill Warren, ameahidi kuzama hadi katika ardhi chini ya bahari na kuutafuta mwili wa kiongozi huyo wa Al-Qaeda, ili kuuthibitishia ulimwengu kuwa aliuawa kweli, limeripoti gazeti la New York Post.

Bwana Warren ambaye amewahi kusaka meli na vyombo vingine vya baharini vilivyozama vipatavyo mia mbili, amesema anataka kuweka wazi ukweli wa jambo hilo.

Bin Laden aliuawa katika mji wa Abbotatabad nchini Pakistan, na wanajeshi wa Marekani, waliosema baadaye kuwa walimzika baharini.

Mzamiaji huyo anatazamia kutumia dola laki nne katika kipindi cha wiki mbili, mwezi ujao atakapoanza msako wake huo.

"Mbona waliuonesha picha za Saddam Hussein?" ameuliza bwana Warren, ambaye rafiki wake wa kike anatokea Urusi, na amemuambia kuwa nchini humo hawaamini kama Osama kweli amekufa.

Majirani wagomvi

Haki miliki ya picha lifehack

Majirani wawili nchini Malaysia waliokuwa wakizozana kila mara walilazimika kutia saini makubaliano ya amani, kama yale yanayotumiwa na nchi zenye migogoro.

Shirika la habari la Reuters limesema mzozo wa majirani hao wanaoishi katika jimbo la kusini la Johor umedumu kwa miaka mitatu, na hata polisi walishindwa kuusuluhisha.

Gazeti la Star limesema, mzozo ulianza kufuatia jirani mmoja kuwa na mbwa waliokuwa wakipiga kelele, na jirani mwingine kujibu mashambulizi wa kufungua muziki kwa sauti ya juu.

Hata hivyo baada ya miaka mitatu ya mzozo uliokuwa ni pamoja na kurushiana taka na hata kugonga mageti kwa kutumia magari yao, wawili hao waliamua kutia saini makubaliano ya maelewano au -- Memorandum of Understanding-- kwa kimombo.

"Ikiwa mmoja wao atavunja makubaliano hayo, mkataba huo wa amani utatumika polisi au mahakamani" amesema msuluhishi wa mzozo huo, Michael Tay.

Bila shaka sasa wataishi kwa amani ameongeza msuluhishi huyo, ambaye pia ni jirani yao.

Mbwa tajiri afariki dunia

Haki miliki ya picha RNLI

Mbwa tajiri kuliko wote duniani amefariki dunia.

Mbwa huyo, aliyejulikana kama Trouble, amekufa akiwa na umri wa miaka kumi na miwili ambao ni karibu sawa na miaka themanini na tano kwa binaadam.

Trouble alifariki akiwa anaishi kifahari huku akihudumiwa kikamilifu na wafanyakazi wake huko Sarasota, Florida, nchini Marekani.

Trouble alipata utajiri wake kufuatia kuachiwa urithi na aliyekuwa mmiliki wake Leona Helmsey aliyefariki dunia mwaka 2007, na kumuachia majumba yake ya kifahari na dola milioni kumi na mbili.

Bi Helmsey alikuwa mjane wa tajiri wa mahoteli, Harry Helmsey, aliyekuwa bilionea.

Katika maisha yake, mbwa Trouble alikuwa akipata vitisho vya kuuawa au kutekwa nyara kutokana na utajiri wake na kulazimika kuwa na ulinzi mkali muda wote.

Fedha alizoacha mbwa huyo sasa zitapelekwa katika wakfu wa Bi Helmsey ambao unasaidia mashirika ya misaada.

Posho yakatwa

Haki miliki ya picha lowcarbnews

Serikali ya Malawi imesimamisha kuwalipa posho maalum wafanyakazi wa serikali wanaoishi na virusi vya UKIMWI.

Kwa mujibu wa BBC, serikali ya Malawi imesema imeacha kuwalipa pesa taslimu, kwa sababu wafanyakazi hao hutumia fedha hizo kwa ajili ya kununulia pombe na makahaba.

Afisa mmoja wa serikali amewatuhumu watu hao kwa kusambaza zaidi virusi vya UKIMWI.

Serikali hiyo imesema, badala yake, wafanyakazi hao wapatao elfu arobaini, sasa watakuwa wakipewa chakula chenye virutubisho kila mwezi badala ya fedha taslimu.

Inakadiriwa kuwa karibu asilimia kumi na tano ya wananchi wa malawi wanaishi na virusi vya Ukimwi.

Nyoka nyumbani

Familia moja nchini Marekani imelazimika kukimbia makazi yao kutokana na nyoka.

Mtandao wa Cnews.com umesema bwana Ben na mkewe Amber walinunua nyumba hiyo mwaka 2009, katika mji wa Idaho.

Hata hivyo nyumba hiyo ilikuwa ina nyoka wengi kiasi kwamba kuna wakati wenye nyumba walikuwa wakihisi ikitikisika kutokana na nyoka hao kuzurura.

Taarifa zinasema mamia ya nyoka walikuwa wanaishi ndani ya ukuta wa nyumba hiyo, na katika maeneo yanayozunguka hapo.

Siku moja bwana Ben aliua nyoka arobaini na wawili.

"Yaani tukasema sasa basi" amesema Ben, ambae wamelazimika kutangaza kufilisika, kwa sababu walinunua nyumba hiyo kwa mkopo wa benki.

"Utadhani tulikuwa tunaishi katika nyumba ya shetani" Amesema Ben.

Benki iliyowakopesha wawili hao hiyo nyumba, imeichukua nyumba hiyi sasa, na tayari imeingizwa sokoni, kwa yeyote anayetaka kuinunua...Na kupafanya nyumbani..

Nywele zaibwa

Haki miliki ya picha network54

Polisi nchini Brazil wamesema mwizi mmoja amemuibia nywele mwanamama mmoja wakati amesimama kituoni akisubiri basi.

Polisi wamesema nyewe la bibie huyo zilikuwa za asili, na ambazo hazijatiwa dawa.

Inspekta wa polisi Jose Carlos Bezerra da Silva amekiambia kituo kimoja cha Televisheni kuwa, mwanamama huyo alikuwa amesimama akisubiri basi katika jiji la Goiania, alipopatwa na mkasa huo.

Mtandao wa Canadian Press umesema mwizi huyo akitumia kifaa kama kisu, alikata nywele za mwanamama huyo, ambazo zilikuwa ndefu kiasi zilikuwa zimepita hata usawa wa kiuno chake.

Mwanamama huyo amesema, alikuwa akidhani mwizi huyo anataka kumuibia mkoba wake.

Polisi wamesema, huenda nywele hizo zimeenda kuuzwa, ili kutengenezewa nywele bandia.

Inspekta Silva amesema hajawahi kuona wizi wa aina hii.

Amesema mwanamama huyo alilazimika kuripoti sakata hilo polisi, kwa sababu za kidini, kwa kuwa angelazimika kumuelezea kiongozi wake wa dini, kwanini nywele zake sio ndefu tena.

Na kwa taarifa yako...... Bundi ana kope tatu za macho.

Tukutane Wiki Ijayo.... Panapo majaaliwa...