Mzozo Abyei majeshi yote kuondoka- Mbeki

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa Sudan Omar al-Bashir na Kiongozi wa Sudan Kusini Salva Kiir

Viongozi wanaohasimiana nchini Sudan wametia saini makubaliano ya kuondoa majeshi yao katika eneo la mpaka lenye mgogoro la Abyei, mpatanishi wa mzozo wa Sudan Thabo Mbeki amesema.

Majeshi ya Kaskazini yalivamia mji huo mwezi uliopita na kuzusha hofu ya kuzuka vita upya, wakati Sudan Kusini ikijiandaa kupata uhuru wake Julai 9.

Vikosi vya pande zote Kusini na Kaskazini vitaondoka katika eneo hilo na nafasi yao kuchukuliwa na wanajeshi wa Ethiopia, alisema Bwana Mbeki.

Awali mpango huu uliripotiwa wiki iliyopita lakini haukuwa umethibitishwa.

Hata hivyo siku mbili baada ya mpango huo kutangazwa, msemaji wa Sudan Kusini alisema majeshi yenye mgogoro yalipigana tena.

Zaidi ya watu 100,000 wamekimbia mapigano katika eneo la Abyei kwa mujibu wa UN.

Wengine 60,000 wamekimbia ghasia katika ya jamii zinazounga mkono upande wa Kusini na vikosi vya Kaskazini katika jimbo jirani la Kordofan Kusini.

Bwana Mbeki, Rais wa zamani wa Afrika Kusini alitangaza mpango huo kupitia mkanda wa video wa Baraza la Umoja wa Matifa kutoka Addis Ababa, mahali mazungumzo yalipofanyika.

Bwana Mbeki alisema pande zote zilitaka mpango huo uanze kutekelezwa mapema, lakini ingetegemea na UN kuruhusu vikosi vyake, Shirika la Habari la AP liliripoti.

"Tunatumaini kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litazingatia makubaliano haya mapema na kuchukua maamuzi haraka ili kwamba vipengele vya makubaliano viweze kutekelezwa” alisema.