Makamu wa Rais FIFA ajiuzulu

Warner, fifa Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jack Warner alikuwa makamu wa Rais FIFA

Jack Warner, makamu Rais wa FIFA ambaye alisimamishwa wadhifa wake kutokana na tuhuma za rushwa amejiuzulu.

Pia amejiuzulu wadhifa wake kama kiongozi wa shirikisho la kandanda kanda ya Amerika ya kaskazini, kati na Caribbean.

Amekuwa ni miongoni mwa maafisa waliotumikia mamlaka ya FIFA kwa muda.

Jack Warner alikuwa anachunguzwa kwa madai ya kuhusika kwake katika kashfa ya kununua kura za wajumbe wa FIFA.

Alikwishasimamishwa uongozi pamoja na Mohammed Bin Hamman, aliyewahi kugombea Urais wa FIFA.

Walishtumiwa kwa kujaribu kuwahonga maafisa wa kandanda wa nchi za Caribbean kabla ya uchaguzi.

Lakini baada ya kutangaza kujiuzulu kwake hatua zote dhidi yake zimesimamishwa.

FIFA imesema kwamba haki yake ya kuchukuliwa kama asiye na hatia imetekelezwa.

Jack Warner amehusika sana na kamati kuu ya utendaji ya FIFA kwa takriban miaka 30.

Aliposimamishwa kazi kwa muda alitishia kuzusha Tsunami katika FIFA akisema Rais Sepp Blatter lazima asimamishwe uongozi.