Libya yasema 15 wauawa kwa mashambulio

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Sorman

Maafisa wa Libya wamesema raia 15- wakiwemo watoto watatu- wameuawa katika shambulio lililofanywa na majeshi ya umoja wa nchi za kujihami za Ulaya NATO kwenye jengo magharibi mwa mji mkuu, Tripoli.

Mwandishi wa BBC aliyechukuliwa na serikali ya Libya kuona eneo hilo kwenye kitongoji cha Sorman alisema jengo hilo lilibomolewa.

Majeshi ya Nato yamesema yanachunguza madai hayo.

Siku ya Jumapili, Nato ilisema kushindwa kufanya kazi kwa silaha huenda ndio iliyosababisha mauaji ya raia katika shambulio la awali mjini Tripoli.

Mhariri wa Mashariki ya Kati wa BBC Jeremy Bowen alipelekwa kuona mabaki ya eneo la makazi ya Khweildy al-Hamidy, mwanachama wa kituo cha mapinduzi ya Libya, ndani ya mtandao wa serikali.

Maafisa wa Libya walimwambia roketi nane zilifanya mashambulio makali kwenye takriban saa 10 au 11 Jumatatu asubuhi.